Thursday, 5 September 2013

Mbowe, Lissu aibu bungeni


THEODOS MGOMBA NA HAMIS SHIMYE, DODOMA
VURUGU kubwa zilitokea bungeni jana na kusababisha shughuli za bunge kusimama kwa zaidi ya nusu saa, baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kukaidi amri ya Naibu Spika, Job Ndugai,
Mbowe aligoma kutoka ukumbini baada ya kukaidi amri ya Naibu Spika aliposimama na kutaka kuzungumza, jambo ambalo Ndugai alimkatalia. Mbowe aliendelea kusimama na kuendelea kubishana jambo hivyo Ndagai kumtaka atoke.



“Nasema toka,” alisema huku Mbowe akiendelea kukaidi na kurudia “Nasema toka.” Baada ya amri hiyo ilizuka vurumai kati ya Mbowe na Wabunge wa CHADEMA upande mmoja na askari wa bunge upande mwingine.
Vurumai hiyo ilidumu kwa takriban nusu saa, ambapo Naibu Spika aliamuru askari kutumia nguvu kumtoa Mbowe bungeni. Hata hivyo, hilo halikuwa jambo rahisi, kwani ziliibuka rabsha na hatimaye Mbowe na wabunge wa chama chake kutoka ukumbini.
Chanzo cha vurumai hiyo ni baada ya kupigwa kwa kura za NDIYO na SIYO, ambapo Ndugai aliamuru kufikiwa hatua hiyo kutokana na kuwepo kwa mvutano baina ya wabunge wanaotaka na wanaokataa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba 2013 kujadiliwa bungeni.
Waliokuwa wakitaka uendelee kujadiliwa walitakiwa kusema SIYO kwa maana ya kupinga kuondolewa, na wale wanaopinga waseme NDIYO kwa maana ya kuondolewa.
Uamuzi wa kura ulitokana na mwongozo aliouomba awali, Ali Khamis Seif (Mkoani - CUF), kumtaka Ndugai kwa mamlaka aliyonayo autoe muswada huo bungeni. Katika mwongozo huo, Ali alitoa sababu kwa nini muswada huo utolewe bungeni.
Hata hivyo, Ndugai alimtaka mbunge huyo asubiri mwongozo huo, ambapo alisema atautolea uamuzi baadaye na kuongeza hakuna kitu kitakacholala na kuendelea kupokea miongozo kwa wabunge wengine.
Ndugai alipokea miongozo ya wabunge wengine, akiwemo Tundu Lissu (Singida Mashariki - CHADEMA), John Mnyika (Ubungo - CHADEMA), Pindi Chana (Viti Maalumu - CCM), Felix Mkosamali (Muhambwe - NCCR Mageuzi), Jenista Muhagama (Peramiho - CCM), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema.
Lissu, Mnyika na Mkosamali waliomba mwongozo unaofanana, ambapo wote walidai muswada huo haujachukua maoni kutoka Zanzibar.
Wakati wabunge hao wakidai hivyo, Pindi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Uongozi alisema si kweli kwa kuwa,  maoni yamechukuliwa na watu wengi walitoa, ikiwemo wananchi na wadau mbalimbali kutoka Zanzibar.
Alisema kamati ilipata maoni kutoka kwa wananchi wa Zanzibar, ikiwemo vyama vya siasa, na tatizo kubwa lilikuwa kutokuwepo kwa wabunge wa kamati yake ilipokuwa ikikutana.
“Tuliwaita wote na ushahidi upo, tatizo tukiwa katika kamati baadhi ya wajumbe walikuwa hawapo na wengine wakifanya kazi zao binafsi Mwanza,’’ alisema.
Jaji Werema kwa upande wake alisema Zanzibar imetoa maoni katika muswada huo, na kwamba binafsi alimwaandikia barua Rais wa Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi,  alijibu barua hiyo kwa kutoa maoni yao.
Kwa mujibu wa Werema, miongoni mwa maoni ya Zanzibar yaliyokuwemo katika barua yao ni kuwepo kwa kipengele cha Rais wa Zanzibar ashauriane na Rais wa Jamhuri katika uteuzi wa wagombea.
“Waheshimiwa wabunge, mawazo ya Zanzibar yapo pamoja na mengine mengi, ambayo kwa kiasi kikubwa yalichangia kupatikana kwa muswada huu. Hivyo Zanzibar wametoa maoni yao,’’ alisisitiza.
Kabla ya Werema kuzungumza, Lukuvi alisimama kutoa mwongozo kuhusiana na hotuba ya Kambi ya Upinzani iliyosomwa juzi na Lissu.
Katika hotuba hiyo, Lissu alidai Rais ameteua watu ambao hawakupelekwa majina yao na taasisi husika katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Lukuvi alisema Lissu amezungumza uongo bungeni na kusema yuko tayari kuleta barua zote za taasisi zilizopendekeza majina ya watu katika tume, endapo atabisha na kukataa kuomba radhi.
“Rais alifanya kama alivyotangaza, watu wote wamechukuliwa na kusema kuwa wawakilishi wa BAKWATA, Jukwaa la Wakristo na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kuwa hawapo si ya kweli na ni uongo dhidi ya Rais Kikwete,’’ alisema.
Aliongeza kuwa: “CHADEMA ilileta majina matatu, likiwemo la Lissu mwenyewe, lakini serikali ikamchukua Profesa Mwesiga Baregu kutokana na usomi na uadilifu wake. Hivyo hakuna taasisi iliyoachwa katika tume,’’ aliongeza.
Baada ya kutoa kauli hiyo, alitaka bunge kutoa adhabu kwa mbunge anayezungumza uongo bungeni, ambapo Ndugai alisema atatoa uamuzi baadaye.
Hata hivyo, Ndugai aliwaambia anaanza kutolea uamuzi wa Ali Khamis Seif, ambapo alisema anawauliza wabunge uamuzi huo wanaupokea au la.
Wakati akiwauliza wabunge, Mnyika alisimama na kumtaka Ndugai kura zihesabiwe na Naibu Spika alisema hamna shaka na kuitaka meza yake ifanye mchakato wa kupiga kura.
Baada ya dakika tatu, kura zilianza kupigwa kwa wabunge wanaokubali hoja ya mbunge wa Mkoani kwa kukubali kwa kusema ‘ndiyo’ na asiyetaka aseme ‘siyo’.
Bunge lenye wabunge 351, wabunge 136 hawakupiga kura jana kutokana na kutokuwepo bungeni, ambapo kura za ndiyo zilikuwa 59 na ‘siyo’ zilikuwa 156 kati ya wabunge 215 waliokuwemo bungeni.
Baada ya kusema kuwa waliosema ‘siyo’ wameshinda na waliosema ‘ndiyo’ wameshindwa na kusema hoja ya mbunge imeshindikana na bunge linaendelea kama kawaida na michango.
Hatimaye Naibu Spika alimwita Augustine Mrema (Vunjo - TLP) kutoa mchango wake juu muswada huo. Aliposimama na kuanza kutoa mchango, Mbowe alisimama na kumuomba Naibu Spika mwongozo.
Hata hivyo, Ndugai alimtaka Mbowe kukaa na kumuacha Mrema azungumze, ambapo Kiongozi huyo alikaidi na kumfanya Naibu Spika kuwataka askari wa bunge kumtoa nje.
Tukio hilo, liliwafanya wabunge wote wa upinzani ambao ni CHADEMA, NCCR-MAGEUZI na CUF, kulisimama kumtetea Mbowe. Ndipo Naibu Spika alipowaita askari ili wamtoe Mbowe.
Askari walipofika walianza kumuomba Mbowe, ambapo wabunge wenzake walisema hapana na kuanza kuimba nyimbo mbalimbali kupinga kutolewa kwake. Tukio hilo, lilichukua dakika tano na askari kuongeza tena nguvu pamoja na makachero wengine waliovaa kiraia na kuanza kutumia nguvu kumtoa.
Nguvu hiyo, ilisababisha kutokea vurugu bungeni, hasa Moses Machali (Kasulu Mjini - NCCR Mageuzi), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini-CHADEMA) na Sylivester Kasulumbayi (Maswa Magharibi - CHADEMA) kumzingira Mbowe.
Hali hiyo ilisababisha matumizi ya nguvu, ambapo askari walimbeba juu Mbilinyi na kumtoa nje, huku Mbunge wa Viti Maalumu, Moza Abeid akilalamika kuvuliwa ushungi.
Baadaye askari walimfuta Kasulumbayi na kumtoa, kabla ya kumaliza na Mbowe, ambaye awali aligoma kutoka na alipoona anafuatwa aliwachukua wabunge wote wa upinzani na kutoka nao, isipokuwa Mrema.
Katika tukio hilo lililodumu kwa takriban nusu sasa, bunge lilikuwa  kama uwanja wa fujo, huku wabunge wengine wakisema ‘wamezoea hao’, ‘watoe nje’, ‘tumewachoka’.
Wakati vurugu hizo zikitokea, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoka ndani ya ukumbi, huku wageni nao wakianza kutolewa, wakiwemo wanafunzi wa shule mbalimbali waliotembelea bunge jana.
Nje nako kulikuwa na ‘vuta nikuvute’ baada ya kuwepo ugomvi mkubwa baina ya Mbilinyi, maarufu kama Sugu na maofisa wa usalama. Hali hiyo ilitokana na Sugu kudai kuwa, kuna ofisa mmoja aliyempiga, ambapo yeye alipomuona alimrukia na kumpiga ngumi na kutaka kupigana naye.
Tukio hilo, lilianzisha rabsha kati ya mbunge huyo na maofisa wa usalama, ambapo wabunge walimchukua Sugu na kumuingiza katika gari la Mbowe na kuondoka naye katika viwanja vya bunge.
Pamoja na rabsha hiyo, Naibu Spika alisema Mbowe na wabunge wake waliofanya karaha hiyo, hawatachukuliwa hatua zozote za kinidhamu, na kwamba alikuwa huru kuendelea na kikao cha bunge ng’we ya jioni.
“Kiti kinamsamehe na kwamba yuko huru kuendelea na kikao baadaye jioni. Tunataka kuonyesha kuwa kiti hakina upendeleo wala hakiwakandamizi wapinzani kama baadhi ya watu wanavyodhani,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru