Wednesday, 4 September 2013

Kesi dhidi ya Pinda kutajwa Sept. 16


NA FURAHA OMARY
KESI ya kikatiba iliyofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), dhidi ya  Waziri Mkuu Mizengo Pinda, imepangwa kutajwa Septemba 16, mwaka huu.
Wanaharakati hao walifungua kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2013, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, wakidai kupinga kauli iliyotolewa bungeni na Waziri Mkuu kwa askari polisi kuwapiga raia wanaokaidi amri halali na kuhatarisha amani.
Kesi hiyo tayari ilishapangiwa Jopo la Majaji watatu wa kulisikiliza, likiongozwa na Jaji Kiongozi Fakihi Jundu. Majaji wengine ni Augustine Mwarija na Dk. Fauz Twaib.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana, Mahakama Kuu, shauri hilo limepangwa kutajwa Septemba 16, mwaka huu, mbele ya jopo hilo la majaji.
Mbali na Waziri Mkuu Pinda, mdaiwa mwingine katika kesi hiyo ni  Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Pinda anadaiwa kutoa kauli hiyo, Juni 19, mwaka huu, wakati wa kipindi cha maswali ya papo hapo, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu, aliyetaka kujua msimamo wa serikali na mambo mengine, malalamiko dhidi ya vyombo vya dola katika baadhi ya maeneo kama Mtwara, kuwapiga wananchi.
Katika hati ya madai, walalamikaji hao walinukuu maneno ambayoyanadaiwa kutolewa na Pinda:
 ìUkifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi, utapigwa tu... Eeh, hamna namna nyingine, eeh maana lazima tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.
ìSasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine, eehÖ maana tumechoka,î inasomeka hati ya madai ikinukuu maneno ya Pinda.
Kupitia hati hiyo ya madai, walalamikaji wanadai kauli na amri kama hizo zinapotolewa na kiongozi mwenye hadhi kama ya mdaiwa wa kwanza (Waziri Mkuu), huchukuliwa kama sheria inayopaswa kutekelezwa na wakala wa utekelezaji wa sheria, kama vile polisi.
Wadai hao wanadai kuwa kwa ufahamu wao, polisi wanaweza kuchukulia kauli hiyo kama amri halali kutoka kwa mkubwa wao na hivyo kuwapiga na kuwatesa watu wasio na hatia, kinyume cha Katiba.
Pia, wanadai kuwa wanatambua kuwa Ibara ya 100 (1) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa kinga kwa wabunge na uhuru wa maoni bungeni.
Aidha, wanadai  wanatambua Ibara ya 100 (2) ya Katiba hiyo ambayo inawawajibisha wabunge wote chini ya masharti ya Katiba na kufafanua kuwa, kauli hiyo aliyoitoa Waziri Mkuu Pinda inakiuka Ibara ya 12(12).
Walalamikaji hao wanaiomba mahakama hiyo itamke kuwa kauli na amri hiyo aliyoitoa Pinda inavunja katiba.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru