Wednesday, 11 September 2013

Kashfa ya kigogo


Na Mwandishi Wetu
UFISADI mkubwa umebainika ndani ya Bodi ya Tumbaku, baada ya Mkurugenzi Mtendaji wake, Wilfred Mushi, kudaiwa kujilipa mshahara na posho mbalimbali kinyume na utaratibu.
Mbali na kujilipa mshahara na posho mbalimbali, ambazo zimepitishwa na Bodi, Mushi anajilipia posho ya pango la nyumba kwa dola za Marekani 1,200, (sh. 1,920,000), tofauti na serikali iliyomtaka aishi katika nyumba yenye gharama ya sh. 400,000.
Uhuru ilifanikiwa kupata nyaraka mbalimbali zilizoonyesha malipo anayojilipa mkurugenzi huyo, ambapo pia anadaiwa kujinunulia samani za ndani vikiwemo vitanda na makochi kwa sh.milioni 23, kinyume na utaratibu.
Pia, nyaraka hizo zinaonyesha kila afanyapo safari kutoka Dar es Salaam kwenda Tabora, hujilipa sh. milioni 2.8 kiasi ambacho ni kikubwa ikilinganisha na kile anachostahili licha ya kupatiwa posho ya mafuta na dereva.
Chanzo chetu cha habari, kilidai kuwa mkurugenzi huyo pia hujilipa sh. milioni tatu kila mwezi kama mshahara, kiwango ambacho bodio hakikitambui.
Kilisema mshahara halali wa bosi huyo ni sh. milioni 2.9, ambazo nazo huzichukua na kufanya kila mwezi awe anajilipa kiasi cha milioni 5.9 kinyume na utaratibu wa ambao Bodi ya Tumbaku imemuidhinishia.
Taarifa zaidi zilidai kuwa Mushi anajilipa sh. milioni 2.7 kama gharama za simu, ambapo alitakiwa kulipwa sh. 400,000 kama malipo stahili kwa huduma ya mawasiliano kila mwezi.
Alipoulizwa kuhusiana na kashfa hiyo jana alipozungumza na Uhuru, Mushi, alisema kila bodi ya mazao ina utaratibu wake inaoufuata kisheria kutokana na uendeshaji wake kujitegemea.
Alisema viwango vya fedha hizo anazojilipa ni haki yake kisheria na zilipitishwa kihalali na bodi.
“Hizo taarifa hazina ukweli na nyaraka zilizopo sizijui kuhusiana na malipo wanayodai, ila nachojua nalipwa sahihi na kama mnahitaji taarifa zaidi, njooni ofisini kwangu Morogoro,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Vita Kawawa, ambaye pia ni Mbunge wa Namtumbo (CCM), alikiri kupitisha malipo hayo na kusema kuwa  mkurugenzi huyo anastahili kulipwa fedha hizo.
“Huo si ufisadi, ni kweli tumemuidhinishia na lazima alipwe kama wakurugenzi wa bodi zingine na hata malipo ya nyumba ni stahili yake kwa kuwa nyumba aliyokuwa anaishi haiendani na hadhi yake,” alisema.
Vita, alisema watu kama hao lazima walipwe hasa ikizingatiwa kuwapata watumishi wa namna hiyo wanaoongoza bodi za mazao ni jambo gumu na yuko tayari kumtetea.
Alidai kuwa matatizo yanayojitokeza sasa yanalenga kumpiga vita mwenyekiti huyo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika nchini.
Alisema Mushi alikuwa miongoni mwa wajumbe wa tume iliyoundwa na serikali kuchunguza ufisadi katika Chama cha Ushirika mkoa wa Tabora.
Hata hivyo, Vita, alisema malipo wanayolalamikia juu ya Mushi, alikuwa analipwa pia mkurugenzi aliyemtangulia.
Habari zilizopatikana kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, zilisema mkurugenzi wa bodi hiyo anapaswa kulipwa mshahara wa sh. milioni 2.9 na uamuzi wa Bodi unatoa tafsiri tofauti juu ya malipo halisi ya Mushi.

000


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru