Tuesday 17 September 2013

Magufuli ataka uchunguzi vituo vya mizani


NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli ameagiza kufanyika kwa uchunguzi kuhusu utendaji wa vituo vya mizani mkoani Iringa.
Magufuli alitoa agizo hilo katika ziara yake ya kikazi mkoani humo katika mkutano wa pamoja na wafanyakazi wa taasisi zinazosimamiwa na wizara hiyo.
Alisema hayo wakati akipokea taarifa za utekelezaji wa majukumu ya kila taasisi mkoani humo na ndipo lilipojitokeza suala la tozo iliyokusanywa kwa magari yaliyokamatwa yakiwa yamezidisha uzito kwa kipindi cha Julai, mwaka huu, katika kituo cha mizani cha Wenda kilichopo kati ya Iringa na Ifunda.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Iringa, Injinia Poul Lyakurwa, alimtaarifu Waziri Magufuli kuwa kiasi cha sh. milioni 31.9 kilikusanywa katika kipindi hicho.
Waziri huyo alishtushwa na kiwango hicho kilichosomwa katika taarifa kuwa kimetokana na magari 735 yaliyokamatwa kati ya magari 20,700 yaliyopimwa sawa na asiliamia 3.5.
ìTakwimu hizi sizikubali, kwani wastani wa magari yanayokamatwa katika nchi nzima unakaribia asilimia 40, iweje barabara kuu kama hii iwe na kiwango kidogo kiasi hicho cha magari yaliyokutwa na makosa, hapa ni lazima pafanyike uchunguzi, hali hiyo hawezi kuiruhusu hata kidogo kuendelea,” alisema.
Katika hatua nyingine,  Waziri Magufuli alimpongeza meneja huyo kwa kufukuza wafanyakazi 18 katika kituo cha mizani cha Makambako kwa kutokuwa waaminifu katika kazi zao.
Waziri huyo alibainisha kuwa takriban asilimia 70 ya wafanyakazi waliokuwa katika vituo mbalimbali vya mizani katika barabara nchi nzima wamebadilishwa baada ya kukamilika kwa kazi ya  kutangaza nafasi hizo upya.
Alisisitiza kuwa wizara hiyo itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali, zikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB), Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na hata kutumia makondakta na wasaidizi katika magari ya usafirishaji ili kuendelea kubaini mbinu zinazotumika katika vitendo vya rushwa katika vituo vya mizani nchini.
Kwa upande mwingine, Wakala wa Majengo Nchini (TBA) na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), wametakiwa kuwa wabunifu ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru