Tuesday 3 September 2013

Rwanda yajirudi



Na Hamis Shimye, Dodoma
TOZO ya mpya ya malori ya mizigo iliyowekwa hivi karibuni na Rwanda kwa ajili ya magari kutoka Tanzania, imeondolewa baada ya kubainika haikuwa sahihi.
Hatua hiyo, ilifikiwa baada ya serikali ya Tanzania kuingilia kati kutokana na adha iliyoanza kujitokeza kwa malori kutoka Tanzania kukwama katika eneo la Lusungu, baada ya kutangazwa kwa tozo hiyo.
Tozo hiyo ilipandishwa kutoka dola za Marekani 152 (sh. 243,200) hadi dola 500 (sh. 800,000) na kuzua malalamiko miongoni mwa wafanyabaishara na wasafirishaji kutoka Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba, alisema tozo hiyo imeondolewa na sasa malori yote yameruhusiwa kuingia nchini humo kama ilivyokuwa awali.
Kwa mujibu wa Dk. Tizeba, serikali ilipata taarifa kuhusiana na jambo hilo, huku ikielezwa kwamba hatua hizo zilichukuluiwa kutokana na sababu mbalimbali za kiuchumi.
ìSuala hilo tulilisikia na juzi asubuhi tukapata taarifa kuhusiana na magari yetu kuzuiwa mpakani. Niliwasiliana na Waziri wa Usafirishaji wa Rwanda, Profesa Silas Lwakabamba na ambaye alidai hakuna kitu kama hicho na kuahidi kunipa jibu baadaye,” alisema.
Alisema baada ya dakika 10, waziri huyo alimpigia simu na kumweleza suala hilo limejitokeza, na kwamba tamko hilo lilitolewa kwa njia ya mdomo na Waziri wa Fedha na Mipango ya Uchumi wa Rwanda, Claver Gatete.
Hata hivyo, alisema waziri huyo alilifanyia kazi na kuhakikisha tozo hilo linaondolewa na kurudisha utaratibu wa zamani.
ìKwa sasa hakuna tatizo, magari yote yamesharuhusiwa na wafanyabiashara wasiwe na wasiwasi kuhusiana na suala hilo kwa kuwa tayari limeshapatiwa ufumbuzi,íí alisema Dk, Tizeba, na kuongeza kwamba suala hilo, linaendelea kufanyiwa kazi na mawaziri wenye dhamana wa nchi husika.
ìHili si letu ni suala la fedha, lakini upandishaji wa gharama hizi una taratibu zake na hata tulipokutana katika kikao cha Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) lilijitokeza,íí alisema.
Wakati serikali ikitoa kauli kuhusiana na suala hilo, habari za kuaminika kuhusiana na tukio hilo zilidai kuwa, tatizo hilo la bandari linachochewa na moja ya nchi wanachama wa EAC.
ìNi kweli tunajua, lakini si suala la upuuzi, mtu akizungumzia bandari ya Tanzania na zao, ninachowaambia wafanyabiashara walete mizigo yao nchini na fitina za kisiasa haziwezi kufanikiwa katika uchumi,íí alisema Dk. Tizeba.
Tozo ya dola za Marekani 500 (sh. 800,000) iliyoondolewa ilianza kutozwa eneo la Lusungu, ambalo ni umbali wa kilometa 139 kutoka mji mkuu wa Rwanda, Kigali.
Magari ya Rwanda yanayotokea Lusungu kwenda Dar es Salaam hutozwa dola 16 (sh. 25,600) kwa kilometa 100. Kutoka Lusungu hadi Dar es Salaam ni kilometa 1,350.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru