Na Theodos Mgomba, Dodoma
TUME ya Mipango, imesema kumekuwa na mwingiliano wa kimajukumu na kiutendaji kati ya Bunge na Serikali, jambo ambalo linatishia kupoka utalaamu wa watendaji.
Kauli hiyo, ilitolewa jana na Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Dk. Philip Mpango, alipokuwa akitoa mada ya vipaumbele vya mipango mipya ndani ya serikali katika mkutano wa makatibu wakuu wa wizara mjini hapa.
Alisema baadhi ya kamati zimekuwa hata zikipanga tozo na kodi mbalimbali, jambo ambalo lilitakiwa kufanywa na serikali.
ìNinaposikia hivyo hata mimi najiuliza hivi utalaamu huo wa kupanga tozo na hata kodi uko upande gani? Je, bungeni kuna watalaamu zaidi ya huku serikalini?" alihoji Dk.Mpango.
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, baadhi ya hoja zinazotolewa na wabunge kuhusu masuala fulani kwa wizara, zinapofuatiliwa hubainika kuwa na maslahi binafsi.
Alisema hizo ni baadhi ya changamoto katika mabadiliko hayo ya mipango ya serikali, hivyo ni vyema watendaji wakazijua na kujua jinsi ya kupambana nazo.
Kuhusu suala ya maofisa masuhuli katika utendaji wake, alisema kuna umuhimu mkubwa kwa maofisa hao kufuata taratibu za fedha katika mfumo mpya wa serikali wa hivi sasa.
Alisema vitendo vya kuhamisha fedha kwenda kwenye miradi ambayo haikuombewa fedha ni kosa, hivyo vitendo hivyo vinapaswa kuachwa mara moja.
Alisema pamoja na kutohamisha fedha kiholela, makatibu wakuu pia lazima wawe macho kwa kufuatilia miradi mbalimbali wanayoambiwa na watalaamu kabla ya kupitisha fedha.
Dk. Mpango alisema ni vyema sasa katika utekelezaji wa mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ni muhimu kwa Hazina kuwa inatoa fedha katika robo ya kila mwaka.
Alisema pamoja na Hazina kutoa fedha katika kila robo mwaka, vilevile haina budi kuhakikisha kuwa mchango wa serikali katika miradi inayofadhiliwa na wafadhili unaongezeka.
Dk. Mpango alisema kwa sasa mchango wa serikali katika miradi ya wafadhili ni mdogo, ikilinganishwa na wafadhili.
Wakati huo huo, makatibu wakuu nchini wametakiwa kutoogopa kusimamia sheria, kanuni na taratibu na kuchukua hatua za nidhamu kwa wanaotia doa utumishi wa umma.
Pia, wametakiwa kuhakikisha kila kada ya utumishi wa umma inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi unaotarajiwa na wananchi.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliyasema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa faragha wa mwaka wa Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa mjini hapa.
Balozi Sefue alisema makatibu wakuu wana wajibu wa kuboresha sura ya utumishi wa umma machoni mwa wananchi.
Alisema hivi sasa bado wananchi wanaendelea kunung'unika na kuilalamikia serikali kutokana na utendaji usioridhisha wa baadhi ya watumishi wa umma.
ìMkitoka hapa kila mmoja wenu aende kuimarisha utendaji, usimamizi na ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa sera na mipango ya serikali na huduma bora kwa wananchi," alisema Balozi Sefue.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru