Wednesday 4 September 2013

Mtandao wa ngono waiangamiza jamii


NA KHADIJA MUSSA
UHUSIANO wa kingono na wapenzi zaidi ya mmoja ni changamoto kubwa inayoathiri afya na masuala ya kijamii nchini.
Pia, uhusiano huo unatajwa kuwa miongoni mwa vichocheo vya kuenea kwa kasi kubwa ya maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU).
Tabia hiyo hatarishi imejikita ndani ya jamii, hususan mahali pa kazi, shuleni na vyuoni, huku wahusika wakidhani hawapo katika hatari ya maambukizi ya VVU kwa kuwa wako nao kwa muda mrefu.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Donan Mmbando, alisema hayo jana alipokuwa akizindua awamu ya pili ya kampeni ya kupambana na ukimwi ya ëTupo Wangapi? Tulizana’, jijini Dar es Salaam.
Aidha, matokeo ya utafiti wa viashiria vya malaria na ukimwi ya mwaka 2011/12, yanaonyesha kuwa asilimia 21 ya wanaume walio kwenye ndoa walikiri kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja katika kipindi cha mwaka mmoja.
Hata hivyo, serikali imesema licha ya uhusiano huo kusababisha maambukizi ya VVU, uwezo wa kupunguza hatari hiyo ni mkubwa iwapo watu wataachana na mtandao wa ngono na kutulizana na mwenza mmoja mwaminifu.
Dk. Mmbando alisema kampeni hiyo itajikita kuhamasisha watu kujitoa kwenye mtandao wa ngono na kutulizana na kuimarisha uhusiano kati ya wenza.
Alisema uhusiano wa kingono na wapenzi zaidi ya mmoja ni tabia inayosababisha athari kubwa kiafya na kijamii kwa kuwa inasababisha kuenea kwa virusi vya ukimwi kwa haraka.
ìUtafiti unaonyesha kuwa asilimia 21 ya wanaume walio katika ndoa walikiri kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja kwenye kipindi cha mwaka mmoja na asilimia nne ya wanawake walio kwenye ndoa walikiri kuwa na uhusiano wa kingono na mwanaume zaidi ya mmoja,î alisema.
Alisema tabia hatarishi ya kuwa na mahusiano ya kingono na wapenzi wengi imejikita katika jamii, hususan mahali pa kazi, shuleni na vyuoni, huku baadhi yao wakidhani hawapo katika hatari ya maambukizi ya ukimwi kwa kuwa wana wapenzi wengi ambao walikaa nao kwa muda mrefu.
Akifafanua, Dk. Mmbando alisema matokeo ya utafiti wa viashiria vya maralia na ukimwi kwa mwaka 2011/12 yanaonyesha maambukizi ya VVU miongoni mwa wanaume na wanawake wenye uhusiano wa kingono na wapenzi wengi ni asilimia 7.5.
Alisema kiwango hicho ni kikubwa kwa asilimia mbili zaidi, ikilinganisha na kile cha maambukizi ya VVU miongoni mwa wanawake na wanaume wenye uhusiano na mpenzi mmoja, ambapo kiwango cha maambukizi ni asilimia 5.5.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru