NA SULEIMAN JONGO, KAHAMA
KATIBU wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amesema vurugu zinazofanywa na viongozi wa CHADEMA, kutaka kukwamisha mchakato wa katiba mpya ni mbinu za kutafuta hoja za kuwaeleza wafadhili waliowapa mabilioni ya fedha kuharibu mchakato huo.
Nape, aliyasema hayo jana wilayani Kahama, alipokuwa akiwahutubia wakazi wa mji huo katika mkutano wa hadhara.
Alisema, CHADEMA wanafanya vurugu hizo kwa makusudi kwa kuwa wana dhima ya kuwaeleza wafadhili wao namna walivyotumia mabilioni ya fedha walizowapatia.
“Wenzetu nasikia wamepewa mabilioni toka nje kwa kisingizio cha kushiriki mchakato wa katiba, na kama ilivyo kwa vibaraka wengine barani Afrika, lengo la fedha hizo si kufanikisha ushiriki huo, bali kuanzisha fujo na vurugu mchakato usimalizike salama na wao wapate ajenda ya kuzungumza mwaka 2015,” alisema Nape.
Akifafanua, alisema baada ya rasimu ya kwanza kutolewa, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alikwenda nje ya nchi alikokaa kwa muda mrefu, aliporudi, viongozi wa chama hicho walianza kuzunguka na helkopta nchi nzima.
“Babu atueleze alifuata nini nje, na fedha za kuzunguka na misafara miwili tofauti kwa kutumia helkopta alizipata wapi, watuambie je walishatoa mrejesho kwa wafadhili wao?” alihoji Nape.
Alisema waliyofanya wabunge wa CHADEMA bungeni haikuwa bahati mbaya, bali ulikuwa mkakati maalumu unaolenga kutimiza malengo yao.
“Lazima wafanye vituko bungeni ili iwe mjadala na wapate sababu na picha za kuonyesha kwa waliowafadhili kuwa wanapambana.
“Walichokifanya kimo kwenye mkakati wao wa ‘machafuko ya umma dhidi ya dola’, mkakati ambao unaratibiwa kutoka nje na baadhi ya wale waliokuwa wakoloni katika nchi za Afrika wakilenga kusababisha machafuko ili nchi isitawalike,” alisema.
Kwa mujibu wa Nape, kutokana na uhakika wa taarifa hizo, ndio maana CCM ilisisitiza Bunge liendelea kuonyeshwa kwenye televisheni ili wananchi waone kile kinachofanywa na wabunge wa CHADEMA.
Akifafanua hoja ya upinzani bungeni juu ya idadi ya wabunge wa Bunge maalumu la katiba, alisema wapinzani hawana hoja ya msingi, bali wanasukumwa na ubinafsi na ulafi wa madaraka.
Wiki iliyopita, baadhi ya wabunge wa CHADEMA walitwangana masumbwi na maofisa usalama, wakipinga Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kutolewa kwenye ukumbi wa bunge.
Sakata hilo lilianza baada ya Naibu Spika, Job Ndugai, kutoa amri kwa askari kumtoa Mbowe, aliyesimama na kukataa kukaa licha ya amri ya Ndugai, huku akiungwa mkono na wabunge wengine wa CHADEMA.
Mbowe alikaidi baada ya mlolongo wa miongozo ulioombwa na Mbunge wa Mkoani, Ali Khamis Seif (CUF), aliyetoa hoja ya kuahirishwa kwa muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Katiba 2013.
Tuesday, 10 September 2013
Siri nzito zavuja
09:51
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru