Tuesday 3 September 2013

Sheria kodi ya majengo kurekebishwa


WIZARA ya Fedha imesema itashirikiana na serikali za mitaa nchini, kuhakikisha inaleta mapendekezo ya urekebishaji wa sheria ya  ukusanyaji wa kodi za majengo ili iletwa bungeni na kupitishwa.
Hali hiyo inasababishwa na sheria ya ukusanyaji wa kodi za majengo uliokuwa unafanywa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa miaka mitano, kumaliza muda wake tangu Julai, mwaka huu.
Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbenne, alisema hayo jana bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu, ambaye alitaka utayari wa serikali kukasimisha jukumu hilo kwa halmashauri za Jiji.
Naibu Waziri Janeth, alisema serikali kupitia marekebisho ya sheria ya fedha, ilikasimu madaraka ya ukusanyaji, ukadiriaji na uhasibu wa kodi za majengo kwa TRA kama wakala kwa niaba ya halmashauri za serikali za mitaa.
“Hatua ya serikali ilichukuliwa kwa lengo la kuboresha makusanyo ya mapato yatokanayo na kodi ya majengo, pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa serikali za mitaa katika ukusanyaji wa kodi hiyo,’’ alisema.
Alisema tangu ilipokabidhiwa jukumu hilo, TRA ilifanikiwa kuongeza kiwango cha makusanyo kwa halmashauri zote tatu za Mkoa wa Dar es Salaam kwa kiasi cha sh. bilioni 3,891 kwa miaka mitatu, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 41.42.
Hivyo, alisema kwa kuwa sheria za ukusanyaji wa kodi za majengo zilifanyiwa marekebisho kwa kuipa uwezo TRA ambayo imeshamaliza muda wake tangu Julai, mwaka huu, serikali ipo katika mchakato wa kukaa na halmashauri kabla ya kuja na sheria nyingine bungeni.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru