Tuesday 17 September 2013

WAZAZI yaambiwa iache kufanya kazi kwa mazoea


NA STEPHEN BALIGEYA, LUSHOTO
MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi Mkoa wa Tanga, Dk. Edmund Mndolwa, amewataka viongozi wa jumuia hiyo kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wabadilike kulingana na siasa za sasa.
Alisema kuendelea kufikiri kwamba chama ni imara bila kufanya kazi ni kukipa kazi ngumu katika uchaguzi mbalimbali, hivyo wanatakiwa kubuni mbinu mpya na zenye tija kwa chama dhidi ya wapinzani.
Wito huo aliutoa juzi wakati wa ziara yake ya kuwashukuru kwa kumchagua kuwa mwenyekiti wa jumuia hiyo, ambayo anaifanya katika wilaya zote tisa za mkoa huo.
Dk. Mndolwa ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, alisema limekuwa jambo la kawaida kwa wenyeviti na makatibu wa jumuia kufanya kazi zisizoeleweka kwa dhana ya ukubwa wa chama, kitu ambacho kimechangia kukiumiza katika baadhi ya uchaguzi.
Kwa hali hiyo, aliwataka viongozi hao kushuka chini kwa wanachama, kwani huko ndiko kwenye msingi na hazina ya watu wengi ambao ni mtaji wa chama kwa siku nyingi kuliko kukaa ofisini.
“Makatibu acheni kuwa kama miungu watu kwa kutoa maagizo kwa simu, nendeni ngazi za kata na kuona utekelezaji wa ilani yetu unavyosimamiwa na viongozi ngazi ya tawi, ì alieleza Dk.  Mndolwa.
Aidha, aliwaeleza kuwa katika kufanikisha ushindi wa chama katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani na uchaguzi mkuu 2015, lazima makundi yaachwe na wafanye kazi kama timu.
ìHatuwezi kukabiliana na upinzani kwa kuhujumiana, lazima tuwe kitu kimoja tupigane kwa ajili ya chama na sio kwa ajili ya mtu, maana mtu atapita, lakini chama hakiwezi kupita,î alisisitiza.
Pia, alisema makundi hudhoofisha nguvu ya siasa katika chama kwa  kiasi kikubwa, na kutoa nafasi kwa wapinzani kuchukua baadhi ya majimbo, jambo ambalo linapaswa kupigwa vita.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru