Wednesday, 11 September 2013

TAKUKURU yaburuza vigogo wanne kortini



Na Mwamvua Mwinyi, Mafia
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wilayani Mafia, mkoani Pwani, imempandisha kizimbani aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mafia, William Shimwela na wenzake.
Mbali ya Shimwela ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, washitakiwa wengine waliopandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya Mafia, ni Ofisa Utumishi wa halmashauri ya Wilaya hiyo, Julius Kimaro.
Wengine ni aliyekuwa mweka hazina wa halmashauri, Geofrey Kiwelu, ambaye kwa sasa amehamishiwa halmashauri ya Wilaya ya Monduli na aliyekuwa Ofisa Utumishi wa halmashauri hiyo, Uledi Lusasi. Lusasi kwa sasa ni Ofisa Tawala wilaya ya Mafia.
Pia, wamo Ofisa Mipango wa wilaya hiyo, Brenden Kachenje na Mtunza fedha, Hatibu Kwao.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Hassan Makube, Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU, John Sang’wa, aliwasomea washitakiwa mashitaka manne.
Wanadaiwa kutumia nyaraka kwa lengo la kumpotosha mwajiri, matumizi mabaya ya madaraka, kuharibu nyaraka ambazo zingeweza kutumika kama ushahidi dhidi yao na kuisababishia hasara halmashauri ya wilaya hiyo ya sh. milioni 7.5.
Makube, alidai kuwa, washitakiwa walitenda makosa hayo kwa kutumia mamlaka waliyokuwa nayo kama maofisa wa uchaguzi, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Alidai kuwa walitenda makosa hayo kinyume na vifungu vya 22 na 31 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007, sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi, sura ya 200, kama ilivyorejewa mwaka 2002.
Hata hivyo, washitakiwa walikana mashitaka na  upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na uliomba tarehe ya usikilizwaji wa kesi.
Shimwela na wenzake wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti, yakiwemo ya kutia saini bondi ya sh. milioni 10 kila mmoja. Kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa mfululizo kuanzia Oktoba 7, hadi 9, mwaka huu.



Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru