Wednesday, 11 September 2013

JK awatangazia kiama ‘mchwa’



NA PETER KATULANDA, MWANZA
RAIS Jakaya Kikwete amehitimisha ziara yake mkoani hapa na kuwaangazia kiama watendaji wa halmashauri watakaochakachua fedha za ujenzi wa nyumba za walimu.
Aliwasisitiza wananchi kuwa maisha bora hayaji kwa kudondoshewa fedha na wanaotafuta ‘kuhomola’ (kula) kupitia kwa wakulima.
Alisema wengi wao huchakachua fedha hizo kupitia kwenye kilimo cha mkataba, wakiwemo wanasiasa.
Rais Kikwete, alisisitiza kuwa ahadi yake ya kujenga meli na kuboresha huduma za usafiri katika Ziwa Victoria na mengine, si hewa, meli mbili mbadala wa MV Bukoba, zitajengwa.
Alisema hayo jana alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku tano mkoani hapa, kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam.
Alizungumza na viongozi mbalimbali wa Chama na serikali kutoka wilaya zote za mkoa wa Mwanza, wazee maarufu na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini.
Alisema dhamira ya serikali ni kuinua hali za watu katika sura mbili, kuwapa huduma za kiuchumi na kijamii kwa huduma bora ikiwemo maji, umeme, elimu, miundombinu ya usafiri, zahanati na kuwajengea mazingira ya ajira na maendeleo.
Pamoja na dhamira hiyo, Rais Kikwete hakuona mahali popote katika ziara hiyo ambapo wanajishughulisha na maendeleo ya viwanda wakati ni moja ya njia za kujenga uchumi na kukuza ajira.
Alisema kuendelea kuwa na miji ambayo haina viwanda ni matatizo.
“Kuna wengine wamebeba dhana potofu, wanasema maisha bora yako wapi, sisi hatukusema tutagawa pesa…unashinda kwenye pulu, fedha hazitadondoka kwenye toka huko na kuingia mfukoni mwako, ” alisema.
Pamoja na kupongeza jitihada za kilimo, Rais Kikwete alisema kuna hali ya kutoelewana katika kilimo cha mkataba.
Alisema baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa, wanataka kujinufaisha kwa kukipiga vita kilimo hicho, wakati kinamnufaisha mkulima.
Kutokana na hilo, aliuagiza mkoa ukae na wadau wajadili na kupata ufumbuzi wa kilimo hicho.
“Watu wanataka kuhomola tu, tafuteni kwa kula kwingine si kwa wakulima, watu hawataondokana na umaskini kwa kulima mazao ya chakula tu, ambayo hawawezi kuyapandisha bei.
“Wataondokana na mazao ya biashara, nimeona zao la dengu linakubali, lifanyeni kuwa la biashara,” alisema na kuiagiza serikali mkoani hapa ijipange kuhamasisha zao hilo.
Alipongeza jitihada zifanywazo katika sekta ya elimu mkoani humo, na kuwaonya watendaji wa halmashauri za wilaya kutumia fedha za ujenzi wa nyumba za walimu vizuri na wasitafute makandarasi wezi ambao watashirikiana nao kuzichakachua.
Alisema kiongozi mzuri ni yule anayeonea fahari maendeleo ya wananchi wake. Alisema kila halmashauri imepewa sh. milioni 500.
Rais alizungumizia pia njia mbadala ya kuboresha na kujenga reli ya kisasa itakayoweza kuchukua mabehewa mengi.
“Kwenye ziwa shabaha yetu ni kuboresha usafiri, ..Ukerewe kumekuwa na malalamiko ya meli ya Butiama kuwa haitoi huduma sawa sawa, tutalishughulikia, tuliahidi kujenga meli mpya taratibu zinaenda vizuri, mambo yakikaa sawa, tutajenga meli kubwa mbili badala ya Mv Bukoba,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo, alisema hakufurahishwa na kasi ya uboreshaji wa huduma za afya na kwamba, atakutana na watendaji wa Bohari ya Dawa (MSD) na kuangalia matatizo yaliyopo ili waondoe tatizo la upungufu wa dawa katika hospitali mbalimbali mkoani hapa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru