Tuesday, 17 September 2013

Ilboru yafungwa kufuatia jaribio la kuichoma moto


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
SHULE ya sekondari ya vipaji maalum ya Ilboru iliyoko wilayani Arumeru mkoani hapa, imefungwa kwa muda usiojulikana baada ya kutokea kwa tukio la jaribio la kuichoma moto.
Tangazo la kufunga shule hiyo lilitolewa ghafla jana asubuhi na Mkuu wa Shule, Julius Shila baada ya kushauriana na bodi ya shule.
Askari polisi wenye sare na waliokuwa kiraia, walionekana wakifanya doria katika eneo la shule na viunga vyake katika harakati za uchunguzi wa awali kubaini chanzo na wahusika wa jaribo la kuchoma moto shule hiyo yenye sifa ya kutoa viongozi wengi wa kitaifa.
Pamoja na kufunga shule, wanafunzi 10 wamesimamishwa masomo kwa siku 21, huku wenzao wanne wakiwa wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, wanafunzi wote watatakiwa kurejea shuleni hapo baada ya kudahiliwa na wakuu wa wilaya zao.
Katikati ya hofu hiyo, wanafunzi waliohojiwa na mwandishi wa habari hii wakiwa wanarudi makwao, waliwahusisha baadhi ya walimu chuoni hapo na sakata la kutaka kuchoma shule hiyo.
Walidai kuwa vitisho vya kuchomwa moto kwa shule hiyo vilianza mwaka jana, ingawa polisi walifanya uchunguzi, lakini hakuna taarifa zaidi zilizotolewa.
Walisema wiki iliyopita kulikuwa na harufu ya mafuta ya petroli yaliyomwagwa eneo jirani na bweni la shule, tukio ambalo polisi walithibitisha kuwa kweli.
ìBaadhi ya walimu walikiri kuhusika, mwaka jana walikubali shule ilitaka kuchomwa moto, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi sasa na tukio kama hilo limejitokeza tena wiki iliyopita, sasa tunahofia usalama wetu,î alidai mwanafunzi mmoja wa kidato cha tatu.
Kaimu Ofisa Elimu wa Mkoa, Sifael Mollel, alisema katika uchunguzi wa madai hayo unaendelea katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wamepewa likizo.
Alisema kuwepo kwa hofu hiyo na wasiwasi wa kuzuka vurugu ndiko kulikosababisha shule ifungwe kwa muda, licha ya kwamba walikuwa bado hawajamaliza mitihani.
ìUongozi umeamua wanafunzi warudishwe nyumbani kutokana na hofu ya shule kuchomwa moto, wanafunzi walikuwa wakifanya mitihani kabla ya kuanza likizo fupi, lakini kuwepo kwa tishio hilo na kuzuka kwa vurugu, ilionekana ni vema ikafungwa,î alisema.
Alisema kwa kawaida likizo fupi ni ya siku 10, lakini kwa tukio hili wanafunzi hao wamepewa maelekezo ya kwenda kuonana na wakuu wa wilaya zao kwa udahili kabla ya kurejea shuleni.
Akizungumzia vitisho vya moto, alisema wanafunzi hao waliwasilisha barua ofisini kwake wakitoa madai kuwa, baadhi ya walimu walikuwa wanataka kuchoma moto shule hiyo.
Alisema polisi walienda kufanya uchunguzi Ijumaa, ambapo waliona harufu ya petroli iliyokuwa imemwagwa jirani na bweni.
Kaimu ofisa elimu huyo hakutawataja wanafunzi ambao wanahojiwa na polisi wala wanafunzi 10 ambao wamesimamishwa kwa siku 21.
Hata hivyo, Shila alikataa kuzungumza na wanahabari kuhusu matukio hayo na hata alipopigiwa simu, alikuwa akiikata mara baada ya kujitambulisha kuwa ni mwandishi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Liberatus Sabas, alikiri polisi kuwepo shuleni hapo wakati tangazo la kufungwa shule likitolewa, lakini alisema ilitokana na sababu za kulinda usalama.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru