Wednesday 11 September 2013

Utulivu watawala mitihani la Saba


Na Mohammed Issa
WANAFUNZI wanaomaliza elimu ya msingi, jana walianza kufanya mitihani yao huku hali ya utulivu ikiwa imetawala kwenye vituo vingi mkoani Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wanafunzi 868,030, wamesajiliwa kufanya mtihani huo Tanzania Bara, kati yao wavulana ni 412,105, sawa na asilimia 47.47 na wasichana ni 455,925, sawa na asilimia 52.52.
Uhuru, ilitembelea baadhi ya shule katika mkoani Dar es Salaam na kushuhudia wanafunzi wakifanya mitihani yao kwa utulivu na ulinzi ukiwa umeimarishwa.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyanzo, alisema Waziri wa wizara hiyo, Dk.Shukuru Kawambwa, alitembelea baadhi ya shule kujionea hali halisi katika mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema Dk.Kawambwa, alitembelea shule ya msingi Kimara Baruti, Mbezi na kwamba, lengo la ziara hiyo alitaka kujionea namna usimamizi na ulinzi ulivyoimarishwa.
Bunyanzo, alisema kwenye maeneo yote nchini, mitihani inafanywa katika hali ya utulivu na hakuna taarifa zozote mbaya zilizoripotiwa. Masomo yanayofanyiwa mtihani ni pamoja na Kiswahili, Kiingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.
Katika shule za msingi Kijitonyama, Ilala Boma, Kigogo, Ali Hassan Mwinyi, Makumbusho na Mnazi Mmoja, hali ya utulivu ilitawala na ulinzi uliimarishwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru