Tuesday, 10 September 2013

SMZ yajipanga kuziadhibu Gold Star na Philtex


Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema inafikiria hatua ya kuichukulia kampuni ya Gold Star, baada ya meli yake kukamatwa na tani 30 za bangi katika pwani ya Italia.
Pia, imesema taarifa kamiliki kuhusu hatua itakazozichukua dhidi ya kampuni ya Philtex ambayo ilisajili meli hiyo kwa niaba ya SMZ, itatolewa hivi karibuni.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Waziri wa Miundombinu wa Zanzibar, Rashid Seif Suleiman, alisema hajapata taarifa kama kampuni ya Gold Star itashitakiwa au la na kwamba, bado wanaendelea kufikiria hatua watakazozichukua.
Kwa mujibu wa Seif, mpaka sasa kampuni ya Philtex imesajili meli 197 za nje kwa niaba ya SMZ.
Alisema kukamatwa kwa meli hiyo ni ushirikiano uliopo baina ya Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA) na mamlaka zingine za kimataifa.
“ZMA ilitoa ushirikiano wa kutosha kwa Polisi wa Kimatiafa (Interpol), mpaka meli hiyo ikakamatwa,” alisema Waziri huyo.
Alisema kampuni ya Gold Star imekiuka masharti ya usajili ambayo yanazuia meli kubeba silaha, dawa za kulevya, wakimbizi au mzigo wowote wa biashara haramu.
Kukamatwa kwa meli hiyo iliyosajiliwa Zanzibar, kumeitia doa Tanzania kwenye jumuia za kimatifa.
Inadaiwa kuwa kampuni ya Philtex, haitumii kigezo chochote wakati wa kusajili meli na kwamba, inaangalia faida zaidi.
Kufuatia hali hiyo, Juni mwaka huu, nchi za Umoja wa Ulaya (EU), chini ya makubaliano ya Paris, Tanzania ilitajwa kuwa ni miongoni mwa nchi ambazo meli zake si salama.
EU ilitoa tamko hilo, baada ya kubaini meli nyingi zilizosajiliwa na Kampuni ya Philtex kwa niaba ya SMZ, kutokuwa na vigezo vinavyotakiwa kisheria.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru