Tuesday 10 September 2013

JK, Maghembe walishana yamini


NA PETER KATULANDA, NGUDU-KWIMBA
RAIS Jakaya Kikwete na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Magembe, wamekula yamini kuhakikisha kuwa maji yanafika mjini Ngudu, katika kipindi cha miezi sita.
Walikula kiapo hicho juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa soka mjini Ngudu, baada ya ‘kilio’ cha Mbunge wa jimbo la Kwimba, Shanif Mansoor, na kelele za wakazi wa jimbo hilo za kutaka watatuliwe kero ya maji, ambayo imedumu kwa muda mrefu.
Kabla ya yamini hiyo, wabunge Mansoor (Kwimba) na Richard Ndassa (Sumve), walivutana vikali mbele ya Rais Kikwete, huku Ndasa akitaka mradi wa maji utekelezwe kutoka Magu ili vijiji 40 vya jimbo lake vipate maji na Mansoor ‘akililia’ maji ya kwenda mjini Ngudu yatoke chanzo cha Ihelele kupitia jimboni kwake.
Akihutubia mamia ya wakazi wa mji huo na vitongoji vyake, Rais Kikwete alisema “Maji kwanza, mengine baadaye.”
Huku akishangiliwa umati uliofurika kumsikiliza, kabla ya kumuita Profesa Magembe, alimwambia, “Haya waziri wa maji njoo ueleze Wizara yako itakavyo tatua kero ya maji hapa.”
Profesa Maghembe, alisema mji wa Ngudu utapatiwa maji kutoka chanzo cha mradi wa Ihelele, unaotekelezwa na KASHUWASA.
Alisema mahitaji ya maji katika mji huo ni mita za ujazo 1500, lakini kwa sasa unapata mita za ujazo 265, sawa na asilimia 22.
Alisema serikali itatoa sh.milioni 500 kwa ajili ya kuchimba mtaro na kutandaza bomba lenye ukubwa wa nchi 8, kutoka kwenye tangi la Mhalo hadi Ngudu mjini, ndani ya miezi sita ijayo.
Waziri huyo, alisema wanalenga kuona wakazi hao wanaanza kufaidika na maji ya ziwa Victoria, ambapo vijiji zaidi ya 13 vitanufaika.
“Tuweke yamini mimi na wewe ili tuje hapa baada ya miezi sita kushuhudia maji hayo, isije kuwa ni ahadi hewa,”  alisema Rais Kikwete.
Profesa Maghembe alijibu: “Mheshimiwa Rais, si ahadi hewa, maji yatafika hapa, tayari wataalamu wameishaandaa ramani ya mradi huo kuwa utatekelezwa ndani ya miezi sita ijayo.”
Rais Kikwete alimuita Mtemi wa Sungusungu wa wilaya ya Kwimba, Shimbi Mogan, ili ashuhudie namna wanavyolishana yamini hiyo, kitendo kilichosababisha umati kuangua vicheko na nderemo za shangwe.
Rais Kikwete alisema miradi yote ni muhimu kwani iwapo maji yatatoka Magu, vijiji 40 vya Ndassa vitapata kupitia Sumve, Malya na Mwanuzi hadi Ngudu.
Awali, Mhandisi wa Maji wilayani humo, Boaz Philipo, na Mkuu wa wilaya hiyo Seleman Mzee, wakitoa taarifa kwa Rais Kikwete, walisema maji ni tatizo na kwa mji wa Ngudu, wanaopata maji safi na salama ni watu 11,310 ambao ni sawa na asilimia 44.6.
Alisema mradi wa kutoka Kijiji cha Mhale–Runele, ndio utakaoharakisha kufikisha maji katika mji huo mkongwe.
Tayari visima virefu vitano ambavyo vilichimbwa kati ya miaka 27 na 57 iliyopita miundo mbinu yake imechakaa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru