Thursday, 5 September 2013

Ambulensi yabambwa na mafuta ya wizi


NA MARCO KANANI, GEITA
MATUMIZI ya magari ya serikali kutumiwa katika matukio ya uhalifu yamezidi kushamiri, ambapo gari la kubebea wagonjwa la Halmashauri ya Wilaya hapa, limebambwa likiwa na mafuta ya wizi.
Kubambwa huko kumetokea wiki chache baada ya gari nyingine ya polisi kukamatwa hivi karibuni, ikiwa imebeba meno ya tembo wilayani Kiteto, Manyara.
Gari hilo la halmashauri, aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 671 AKW, lilikamatwa jana, usiku wa manane likiwa limebeba mafuta yanayodaiwa kuibwa katika mgodi wa dhahabu unaomilikiwa na Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM).
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Leonard Paul, alisema gari hilo linalotoa huduma katika Kituo cha Afya cha Nzera, lilikamatwa na walinzi wa mgodi huo, saa saba usiku wa kuamkia jana, katikati ya mgodi na eneo la Geita Power likiendeshwa na Hamud Bihemo (28), mfanyakazi wa halmashauri hiyo.
Alisema gari hilo lilikuwa na watu wanane, wakiwemo wafanyakazi wa mgodi huo, wakiwa wamepakia mapipa matatu ya dizeli yenye ujazo wa lita 630 zenye thamani ya sh. 1,686,000, mali ya mgodi huo.
Kamanda Paul aliwataja watu wengine waliokamatwa kuhusiana na wizi huo kuwa, Selemani Magoso (31) ambaye ni dereva wa bodaboda, Malemo Paulo (38), Julius Boaz (28) na Rashid Hussein (27) mlinzi wa mgodi huo.
Wengine waliotiwa mbaroni ni Ismail Zuberi (26) mlinzi wa Kampuni ya G4S inayolinda mgodini hapo, Christopher Kombo (30) na Joseph Christopher, wote wakiwa waendesha mitambo mgodini hapo.
Kamanda Paul alisema pamoja na kukutwa wameshapakia mapipa matatu, katika eneo la tukio kulikuwa na mapipa mengine manne ambayo pia yalikuwa yapakiwe ndani ya gari hilo tayari kuvushwa nje ya mgodi.
Alisema gari hilo lilikuwa tayari limewekewa nembo ya utepe wa njano ubavuni pamoja na kuwekewa bendera kama yalivyo magari ya mgodi huo ili lionekane liko kazini.
Watuhumiwa hao, kwa mujibu wa Kamanda Paul, wanashikiliwa katika kituo kikuu cha Polisi Geita wakiendelea kuhojiwa kabla ya kupandishwa mahakamani.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa, Saidi Magalula, alisema ni fedheha kuona gari la serikali linatumika kufanya wizi. Alikemea vikali vitendo hivyo na kuwaagiza wakurugenzi kufuatilia magari ya serikali ili yasitumike vibaya.
Magalula alisema gari hilo lilitolewa na GGM na kukabidhiwa kwa halmashauri ili lisaidie huduma za afya katika kituo hicho, hivyo kutumika kuuibia mgodi  uliolitoa ni dhihaka kwa waliofanya hivyo, na kusisitiza kuwa lazima sheria kali zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru