Tuesday 10 September 2013

BAADA YA MKE KUGOMA KUUZA MALI


Mhamiaji haramu ajinyonga

Na Angela Sebastian, Bukoba
RAIA wa Rwanda, France Mathias, amejinyonga hadi kufa wilayani Kyerwa mkoani Kagera, baada ya mkewe kukataa kuuza mali na kuondoka nchini.
Huo ni utekelezaji wa operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu inayoendelea nchini hivi sasa.
Kwa mujibu wa binti wa marehemu, Melania France, tangu kuanza kwa operesheni kimbunga ya kuwasaka wahamiaji haramu, wazazi wake waliingia katika mzozo mkubwa, ambapo baba alitaka wauze mali zote na kuondoka.
Hata hivyo, Melania, alisema mama yake ambaye ni mwenyeji wa wilaya ya Ngara, alimkatalia mumewe na baadaye mama huyo alitoroka usiku akiwa na watoto watatu.
Alisema pia anafahamu marehemu baba yake alikuwa na uwezo na mwenye fedha, ingawa hakufahamu anapozihifadhi.
Alisema kuna wakati alitishia kuwaua baada ya kuibuka mzozo kwenye familia yao.
Joseph Leo, ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kikukulu, alisema Mathias alikuwa katika orodha ya wahamiaji haramu iliyoandaliwa na uongozi wake.
Alikiri kufahamu ugomvi ulioibuka ndani ya familia ya marehemu, baada ya oparesheni hiyo kuanza.
Leo, alisema Mathias alifika eneo hilo tangu mwaka 1976.
“Nilipofika eneo la tukio nilikuta Mathias amejinyonga chumbani kwake, huku kukiwa na idadi kubwa ya noti za sh.5,000 na sh.10,000 zinazokadiriwa kufikia sh.milioni saba zikiwa zimechanwa vipande vipande,” alisema Leo.
Naye Ofisa Tarafa ya Kituntu, Nicholaus Rugemalira, alisema marehemu alikuwa raia wa Rwanda.
Alisema taarifa alizozipata zilidai kuwa marehemu alikuwa na mpango wa kuiteketeza familia yake kwa moto au panga, lakini mkewe aliubaini, ndipo aliamua kutoroka usiku na watoto wake watatu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi, alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo, alisema hana taarifa kamili na aliahidi kulifuatilia.
Hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete, aliamuru wahamiaji haramu nchini kujisalimisha ndani ya wiki mbili kuanzia Agosti 26, kabla ya kuanza kwa operesheni ya kusaka silaha na wahamiaji haramu.
Alitoa amri hiyo wakati akihutubia wakazi wa mji wa Biharamulo, mkoani Kagera, kutokana na matukio ya mara kwa mara ya ujambazi katika mikoa ya Kagera na Kigoma.
“Nawaamuru majambazi wote, wenye kumiliki silaha kinyume cha sheria na wahamiaji haramu wote, wajisalimishe katika wiki mbili kuanzia leo.
“Wajisalimishe wao pamoja na silaha zao. Baada ya hapo, tunaanzisha oparesheni ambayo haijapata kuonekana katika historia ya nchi yetu,” alisema Rais Kikwete.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru