Wednesday 25 September 2013

Kinana arusha kombora zito


NA WAANDISHI WETU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimevitaka vyama vya upinzani kutotafuta umaarufu kupitia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya CCM.
Pia, kimesema kinatekeleza miradi mbalimbali kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wote bila kujali itikadi za vyama.
Wakati CCM kikiendelea kung’ara katika kuwahudumia wananchi, CHADEMA kinazidi kumeguka, ambapo wilayani Handeni kimefutika baada ya wanachama zaidi ya 300 kukihama na kujiunga na CCM, wakiwemo viongozi wake.
Hayo yalijitokeza juzi wakati ya ziara ya Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo, ambapo viongozi na wanachama walikabidhi kadi zao CCM.
Mbali na hilo, Chama kimewataka viongozi wote kuanzia ngazi ya shina hadi taifa kuacha utendaji wa mazoea na kuwa wakali na kuisimamia serikali katika utekelezaji shughuli za maendeleo.
Msiamamo huo ulitolewa jana Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, mjini Musoma, wakati akiwahutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mkendo.
Alisema wapinzani wanapaswa kuacha kimbelembele na kujinasibisha kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanywa na serikali iliyo chini ya CCM kwa kuwa, iko kwenye Ilani na ahadi za Chama kwa wananchi na taifa kwa jumla.
Kinana alitoa mfano wa mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria unaoendelea kujengwa mjini Musoma, ambapo alisema licha ya wapinzani kudai ni wao, lakini ukweli ni kwamba mradi huo ni ahadi ya CCM na sasa inautekeleza.
“Wakati wenzetu wa upinzani wakipita wakidanganya wananchi na kujinasibisha na miradi yetu ya maendeleo, sisi tutaendelea kuitekeleza kwa maslahi ya Watanzania wote,” alisema.
Mbali na mradi huo serikali mkoani Mara, pia inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Rufani ya Kwangwa, inayojengwa wilayani Musoma.
Mapema, akiwahutubia maelfu ya wananchi wa mji wa Shirati wilayani Rorya mkoa wa Mara, Kinana alisema sasa ni wakati kwa wana-CCM kuhakikisha wanakuwa wakali na kuisimamia serikali ili itimize majukumu yake kwa Watanzania.
“Nawaagiza wana-CCM wote kuanzia ngazi ya shina, tawi, kata, wilaya mkoa hadi taifa kuwa wakali na kuibana serikali kuhakikisha inatimiza majukumu yake kwa taifa. Bila kufanya hivyo siku moja itakula kwetu,” alisema.
Kinana alisema serikali ya CCM imefanya mambo mengi kwa Watanzania na kuahidi kuwatumikia kadri iwezekanavyo, hivyo wananchi wanapaswa kuwa makini kutokana na kauli za wapinzani.
Akizungumzia miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo, alisema ndani ya mwaka huu wa fedha serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali.
Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ile ya kusambaza umeme na maji vijijini, ambapo jumla ya vijiji 30 vitanufaika.
Alisema, mbali na miradi hiyo, serikali pia inaendelea na ujenzi wa malambo mawili ya maji katika kata ya Utegi wilayani humo.
Kwa upande wake, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, aliwataka wananchi wa Shirati na Rorya, hususan vijana kutokubali kushawishika na propaganda za wapinzani kuhusu katiba mpya zenye lengo la kuibua mtafaruku katika jamii.
Nape alisema hakuna chama chochote cha siasa kilicho na kauli ya mwisho kuhusu suala hilo, bali wananchi ndio watakaoamua ni aina gani ya katiba wanayoihitaji.
Kwa mujibu wa Nape, viko baadhi ya vyama vya siasa vilivyodai kuungana na kupita mikoani kwa ajili ya suala la katiba mpya, Watanzania wanapaswa kuwa makini na yale watakayoelezwa na watu hao endapo yatakuwa yakiashiria uvunjifu wa amani.
Kinana na Nape wamehitimishisha ziara yao ya kikazi ya wiki tatu katika mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa ya Shinyanga, Simiyu na Mara.
Kutoka Handeni, Mwandishi Wetu anaripoti kuwa, Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo, ameisambaratisha kambi ya CHADEMA baada ya ëkukombaí wanachama 380 wa chama hicho, ukiwemo uongozi wa juu wa wilaya.
Uamuzi wa viongozi na wanachama hao kujiunga na CCM, umeelezwa kuwa wa kihistoria kwa chama hicho wilayani humo tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.
Wanachama na viongozi hao walichukua uamuzi huo baada ya kukabidhi kwa Bulembo kadi zao za uanachama na nyaraka zote muhimu za kuendeshea ofisi ya wilaya hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliyofanyika juzi katika Kata ya Kwamatuku.
Viongozi hao ni pamoja na Mwenyekiti wa Wilaya hiyo, Luka Selemani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Maguruwe, Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa na Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Wilaya.
Wengine ni Katibu wa wilaya hiyo Athumani Ngido, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa na Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Wilaya na Mkoa wa Tanga, Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa ya Wilaya hiyo, Jackson Francis, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kata ya Kabuku Nje na aliwahi kuwa mgombea udiwani katika uchaguzi mkuu uliopita.
Mbali na hao, wamo Mwenyekiti wa BAVICHA tawi la Kwamatuku, Abraham Mtengwa na mjumbe wa kushughulikia migomo ya chama hicho Juma Mkomba.
Akihutubia wananchi katika mkutano huo wa hadhara, Bulembo alisema kukimbia kwa viongozi na wanachama hao ni ishara kuu ya chama hicho kusambaratika katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.
Alisema kadri siku zinavyoenda, CHADEMA itazidi kusambaratika kutokana na baadhi ya viongozi wake kukumbatia madaraka, huku wengine wakiachwa kuwa wapigadebe tu.
ìDhambi ya umimi, udugu na urafiki utaimaliza CHADEMA, kwani kwa mtu mwenye akili timamu hawezi kubaki ndani ya CHADEMA akitazama wanandugu wakigawana vyeo.
ìMaana yake nini... kama huna baba, mama au mjomba huwezi kupata cheo ndani ya CHADEMA na ili kuamini hilo angalieni wabunge wao wa viti maalumu jinsi walivyoteuliwa ëkiudugu na kiushikajií,î alisema Bulembo.
Alisema wabunge hao wa viti maalumu hawakuteuliwa kulingana na matokeo ya ushindi iliyoupata CHADEMA katika mikoa mbalimbali, bali umelenga maeneo wanakotoka viongozi wakuu wa chama hicho.
Kwa upande wake aliyekuwa Katibu wa wilaya hiyo, Ngindo, alisema kuhama kwao katika chama hicho ni pigo kwa CHADEMA.
Ngindo alisema waliamua kufanya uamuzi mgumu wa kukihama chama hicho kutokana viongozi wake wa juu kujithamini wenyewe bila kujali wengine waliopo katika wilaya.
ìHiki si chama, bali ni kampuni inayojiendesha kwa kujali maslahi binafsi. Kama kingekuwa chama cha siasa, basi hivi sasa tungekuwa mbali, hususan katika wilaya hii,î alisema.
Naye Selemani aliyekuwa Mwenyekiti wa Wilaya hiyo, alisema kuanzia sasa watapanga mikakati ya kukifuta chama hicho ili kisisikike katika wilaya hiyo.
ìHandeni unapoitaja CHADEMA maana yake unataja kikosi hiki kilichorudi leo CCMÖ sasa kazi moja tu kuhakikisha kila mtu aliyekuwa CHADEMA anarudi CCM kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa hapo mwakani,î alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru