Wednesday, 4 September 2013

Wanaodaiwa kumuua bilionea Arusha kortini


Na Rodrick Makundi, Moshi
SHUGHULI katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini hapa, jana zilisimama kwa takriban dakika 15, kutokana na vilio vya ndugu wa marehemu, bilionea Erasto Msuya, baada ya kufikishwa kwa washitakiwa wanaotuhumiwa kumuua mfanyabiashara huyo.
Ndugu hao wakiwemo dada wa marehemu, walipowaona washitakiwa hao waliangua vilio vilivyosababisha kelele na hivyo mwenendo wa mashauri katika mahakama kusimama.
Washitakiwa waliofikishwa mahakamani hapo, ambako kulikuwa na ulinzi mkali wa askari, wakiwemo wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU), waliokuwa na silaha ni Sharifu Mohamed na Musa Mangu.
Hata hivyo, mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo ya mauaji ya Msuya (43), Shaibu Mpungi, hakufikishwa mahakamani hapo, akitokea mahabusu kwa sababu zinazodaiwa kuwa na maradhi, ambayo hata hivyo hakuyataja.
Baada ya kufikishwa mahakamani hapo, saa tano asubuhi, washitakiwa hao walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Theotimus Swai, ambapo shauri hilo liliahirishwa ndani ya dakika 10.
Dada wa Msuya, Antuja Msuya na Bahati Msuya wote wakazi wa mkoani Arusha na Mererani mkoani Manyara, walipowaona washitakiwa hao walishindwa kuvumilia na kuangua kilio hadi kuzimia, kitendo kilichovuruga mwenendo wa mashauri yaliyokuwa yanasikilizwa mahakamani hapo.
Mbele ya Hakimu Swai, Wakili wa Serikali Stella Majaliwa, alidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Kwa upande wake, Wakili wa Utetezi Hudson Ndusyepo, anayewatetea Mohamed na Mangu, aliiomba mahakama kuamuru upande wa Jamhuri kuharakisha upelelezi kwa misingi ya kuwatendea haki washitakiwa ambao wamekuwa wakiteseka rumande.
Hakimu huyo aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 18, mwaka huu, kwa kutajwa na washitakiwa walirudishwa rumande.
Mohamed, Mpungi na Mangu wanadaiwa kumuua Msuya katika tukio lililotokea Agosti 7, mwaka huu, saa sita mchana, kando ya barabara kuu ya Arusha/Moshi katika eneo la Mijohoroni, wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru