Tuesday, 3 September 2013

Uchumi wetu unakuwa, sarafu iko imara -BoT


Na Peter Orwa, Bagamayo
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Profesa Benno Ndulu, amesema Watanzania hawana sababu ya kuwa na hofu ya uchumi wa nchi yao, kwani uko imara.
Aidha, amesema uchumi huo umezidi kukua na sarafu yake ndio inaongoza kwa uimara katika ukanda wa Afrika Mashariki, dhidi ya mfumuko wa bei.
Pia, Profesa Ndulu alisema BoT imeanza mchakato wa kuboresha utendaji wa benki za biashara nchini, kwa kuunda chombo maalumu cha kupitia rekodi ya usafi wa mkopaji, huku benki hizo zikiongezewa kiwango cha mtaji wanachostahili kisheria ili kufanyia biashara.
Gavana alitoa kauli hizo za ufafanuzi, juzi alipokuwa akifungua semina maalumu ya BoT kwa waandishi wa habari mjini hapa, kuwaelimisha majukumu ya chombo hicho inayofanyika kwa siku tano katika hoteli ya Stella Maris.
Profesa Ndulu alisema uchumi uliopo sasa nchini ni imara na unakuwa kwa kasi kubwa ya asilimia 7.4, kiwango kilicho juu kuliko baadhi ya nchi zinazotajwa zina kasi kubwa ya ukuaji uchumi duniani, akitoa mfano wa India.
Aliisifu serikali kwa kuweza kudhibiti uimara wa sarafu yake kwa zaidi ya mwaka sasa, baada kukumbwa na msukosuko mkubwa mwaka juzi.
Bila ya kutaja kiwango, alisema hivi sasa kuna ujazo wa kutosha wa fedha za kigeni uliowezesha mfumuko wa bei uliofikia asilimia 18 awali na sasa kuwa chini ya asilimia 10 na kuna dalili za kupungua zaidi. Thamani ya sarafu zilishuka kutokana na athari za mdororo wa uchumi duniani.
Profesa Ndulu alitaja baadhi ya bidhaa zinazoumarisha uchumi wa nchi kwa sasa kuwa dhahabu, ambayo iko juu katika kuongeza ujazo wa fedha za kigeni na bei yake iko juu sokoni, huku zao la kahawa likianza kupata bei nzuri katika soko la dunia, baada ya kuyumba kwa muda.
ìHali ya uchumi ni nzuri, lakini hatujafika. Safari ni ndefu,î alisema Profesa Ndulu ambaye kitaaluma ni mchumi, wakati akitoa maoni yake ya jumla kuhusu hali ya uchumi wa nchi ulivyo kwa sasa.
Kuhusu benki za biashara, Profesa Ndulu alisema BoT imeanzisha mikakati ya kuimarisha huduma za taasisi hizo zilizo chini yake, kwa kuundwa kwa chombo maalumu cha kutunza taarifa zinazosaidia kuwatathmini wakopaji kwa lengo la kulinda usalama wa mikopo hiyo.
Miongoni mwa taarifa hizo za kutathminiwa kwa mujibu wa Profesa Ndulu ni pamoja na rekodi binafsi za alivyokopa awali, uhalifu na maisha binafsi ya mkopaji.
Alisema, BoT imeongeza kiwango cha mitaji ambayo benki inastahili kuwa nayo kutoka sh. bilioni tano za sasa hadi sh. bilioni 15 ifikapo mwaka 2015, ili kudhibiti uimara wa utendaji wa vyombo hivyo, huku akisistiza hadi sasa nyingi za benki hizo ambazo jumla yake ni 51 nchini, zimeshafikisha kiwango hicho.
Naye, Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi wa BoT, Dk. Joseph Massawe, alisema suala la watu kufanya biashara za chenji ya sarafu, ikiwemo katika vituo vya mabasi kama vile daladala ni batili kwa kuwa taasisi hiyo imeweka utaratibu wa watu kununua chenji kutoka benki hiyo bila ya gharama za ziada.
Dk. Massawe, alisema hivi sasa BoT inaweka mkakati wa kupambana na tatizo hilo, ingawa hakutaka kufafanua hatua zitakazochukuliwa.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, benki nyingi za biashara zimekuwa zikitakiwa kununua fedha hizo za sarafu kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa chenji, lakini zinazembea, hata pale zinapopewa kwa kulazimishwa, nao huzirudisha wakati wa kuweka fedha BoT.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru