Tuesday 24 September 2013

Polisi yanasa maiti yenye dawa za kulevya

Na Mwandishi Wetu
POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inawashikilia Nasri Rajabu ëRobotí na Mwanaisha Kapama, wakazi wa Kigogo Luhanga, wakiwa na maiti ya mfanyabiashara Rajabu Rajabu ikiwa na dawa za kulevya.
Watuhumiwa hao wamekamatwa siku moja baada ya gazeti hili kuripoti habari ya kufariki kwa mfanyabiashara huyo, baada ya pipi 33 za dawa za kulevya alizokuwa amezimeza, kumpasukia tumboni.
Kufa kwa Rajabu kumeibua mambo mazito, baada ya polisi kudai taarifa zinaonyesha kuwa, alikuwa mhalifu mzoefu wa usafirishaji wa dawa za kulevya na kabla ya kurejea nchini, alikuwa akitumikia kifungo barani Asia.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova alisema jana, wamekamata pipi 33 za dawa za kulevya aina ya Heroine zenye thamani ya mamilioni ya fedha.
Alisema baada ya polisi kupata taarifa ya tukio hilo, walikwenda nyumbani kwa Rajabu maeneo ya Tabata na kumhoji, ambapo waligundua uwepo wa maiti sebuleni, ikiwa imelazwa chali katika godoro.
Kwa mujibu wa Kova, Rajabu ndiye mmiliki wa chumba kilichokutwa maiti na uchunguzi unaonyesha marehemu alifika juzi kutoka Mtwara.
Alisema imebainika kuwa kabla ya kifo cha mfanyabiashara huyo, alikwenda bafuni kuoga na alirudi katika chumba hicho na ndipo alipokutwa na umauti.
Kamishna huyo alisema mazingira ya kifo hicho ndiyo yaliyosababisha polisi kupata taarifa na walipofika eneo la tukio, waliuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa uchunguzi.
Alisema mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na madaktari wawili, ukishuhudiwa na maofisa wa polisi na ndugu za marehemu, na kwamba alikutwa na pipi 33 za dawa za kulevya.
Kova alisema uchunguzi unaendelea ili kubaini mtandao wa usafirishaji wa dawa hizo, ambao umehusisha marehemu na watakaokamatwa watachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema marehemu alikutwa na hati ya dharura ya kusafiria ambayo haikuonyesha anasafiri kwenda nchi gani.
Kova alisema marehemu alikutwa na vitu mbalimbali, ikiwemo fedha taslimu za Kenya sh. 700, dola 100 za Marekani (sh. 160,000), pamoja na fedha za Shelisheli 100.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru