Wednesday 18 September 2013

Kikwete awazodoa wanasiasa waongo

Na Mwandishi Wetu, San Francisco, California
RAIS Jakaya Kikwete ameshangazwa na kiwango cha uongo cha baadhi ya wanasiasa, hasa madai kuwa aliteua wajumbe wa Tume ya Katiba bila kuongozwa na mapendekezo ya wadau mbalimbali waliopendekeza majina hayo.

Aidha, amesema kuwa bado anaendelea kuamini kuwa mchakato wa Katiba Mpya utafikia mwisho wake mwakani, hivyo kuiwezesha Tanzania kufanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 chini ya Katiba Mpya.
Vilevile, Rais Kikwete amesema kuwa hana tatizo na watu wanaopinga sera za serikali au hata kumpinga yeye binafsi, bali tatizo lake ni wanasiasa na wanaharakati wanaochochea ghasia, fujo na uvunjifu wa amani.
Rais Kikwete aliyasema hayo juzi, mjini San Rafael, California, alipokutana na kuzungumza na jumuia ya Watanzania waishio jimbo hilo nchini Marekani, wakati alipoanza ziara yake ya siku mbili, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Marekani.
Katika hotuba yake, ambapo alizungumzia mambo mbalimbali, Rais Kikwete aligusia mjadala wa karibuni Bungeni kuhusu mchakato wa Katiba Mpya na kusema kuwa, alishangazwa na madai kuwa yeye kama Rais hakuongozwa na mapendekezo ya wadau wakati anateua Tume ya Katiba.
“Watu wote niliowateua walipendekezwa na wadau mbali mbali, zikiwemo taasisi za dini. Yule Mama Maria Kashonda alipendekezwa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Mama Mwantumu Malale alipendekeza Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
“Kila kundi ambalo lilipendekeza watu limepata mjumbe katika tume hiyo, wakiwemo walemavu ambao naambiwa nimewasahau,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Hivi nyie wanasiasa wenzangu mkikosa hoja mnaongopa hata kwa vitu ambavyo viko wazi kabisa. Tulikubaliana kuwa Rais angefanya uteuzi wa wajumbe wa tume baada ya kupokea mapendekezo ya wadau mbali na katika mchakato ulioendeshwa kwa uwazi kabisa. Hivyo, ndiyo ilivyofanyika. Sasa uongo wa nini? Kama hakuna hoja ni kwamba hakuna tu na wala uongo hautasaidia.”
Kuhusu kama Tanzania itaweza kupata Katiba Mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Rais Kikwete amesema: “Ningependa sana, na kwa kweli ni matarajio yangu makubwa kuwa, tuweze kumaliza mchakato wetu mwaka 2014 na tuweze kuwa na Katiba Mpya ili iongoze Uchaguzi Mkuu wetu wa mwaka 2015.
‘’Mchakato wetu unakwenda vizuri na wala siyo lazima tuhangaike na Katiba kwa miaka mingi. Muhimu ni ushirikishwaji wa kila mmoja wetu.”
Akizungumzia tabia za wanasiasa wa Tanzania kwa jumla, hasa wale wanaochochea chuki na ghasia, Rais Kikwete aliwaambia Watanzania hao:
“Sina tatizo na wanasiasa au wanaharakati kupinga sera za serikali yangu. Hili ni suala la nguvu ya hoja na tunao uwezo mkubwa wa kutetea sera zetu. Na wala sina tatizo na watu kunipinga mimi binafsi. Kinachonipa taabu ni pale wanasiasa na wanaharakati wanapochochea ghasia na kuleta fujo. Kama mtu anataka kuongoza Tanzania si asubiri hadi atakapochaguliwa?”
Rais Kikwete aliongeza: “Hivi unapochochea ghasia, fujo na chuki na kweli mambo hayo yakatokea na nchi ikateketea, utaongoza nchi ya namna gani? Utaongoza magofu na majivu yatakayobakia baada ya nchi kuteketea?”
Kuhusu mjadala wa karibuni kuhusu kama Rais awe na madaraka ya kuteua wajumbe 166 wa nyongeza ili kuingia katika Bunge la Katiba kujadili Rasimu ya Katiba Mpya, Rais Kikwete alisema kuwa yeye hana taabu kama itabidi ateua basi atateua, lakini kama siyo lazima yeye hana taabu.
“Mimi sina taabu, wakisema niteue, basi nitateua. Wakisema nisiteua vilevile sina taabu, isitoshe hiyo itakuwa inanipungumzia mzigo na kazi. Ile kazi yenyewe ya kuteua wajumbe wa Tume ya Katiba haikuwa rahisi.”
Rais Kikwete alitumia siku ya pili ya ziara yake katika Jimbo la California kwa kutembelea Jiji la Vallejo, ambako alikutana na Meya wa Mji huo, Osby Davis, pamoja na madiwani wa jiji hilo na wafanyakazi wake.
Ziara hiyo ya Rais Kikwete katika Jiji la Vallejo, nje ya Jiji la San Francisco, imekuja wakati wa Kumbukumbu ya Miaka 20 tangu jiji hilo lianzishe uhusiano wa kidada na mji wa Bagamoyo ulioko mkoa wa Pwani ulioanzishwa mwaka 1993.
Rais Kikwete alitumia muda mwingi wakati wa mkutano na baadaye wakati wa chakula cha mchana na viongozi wa jiji hilo kujenga hoja ya kuvutia wawekezaji wa Jiji la Vallejo kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Pia, Rais Kikwete aliwaelezea viongozi wa jiji hilo kuhusu historia ya mji wa Bagamoyo na asili ya jina la mji huo lilitokana na enzi ya watumwa ambako mji uliitwa Bwaga Moyo (Tuliza Moyo Wako).
0000
...awatosa wauza unga
“Ukikamatwa na dawa za kulevya hatukutetei, hatuwezi kuendelea kuwa na sifa ya kufanya biashara za ovyo ovyo kiasi hicho.
Na Mwandishi Wetu, San Francisco, California
RAIS Jakaya Kikwete amesema serikali yake haitawatetea Watanzania wanaokamatwa wamebeba dawa za kulevya nje ya nchi kwa sababu biashara hiyo ni haramu.
Aidha, amesema kuwa serikali yake haina uhakika kama suala la uraia pacha (dual citizenship) litaweza kuwemo katika Katiba Mpya kwa sababu suala hilo halikuwamo katika Rasimu ya Katiba hata kama limependekezwa tena na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais Kikwete amesema ni wajibu wa Watanzania wanaoishi ughaibuni kuwa raia wema na kufuata na kuheshimu sheria katika nchi wanazoishi kwa sababu wakivunja sheria za nchi hizo serikali yake haitawatetea.
Alitoa ufafanuzi huo juzi alipokutana na kuzungumza na Watanzania wanaoishi katika Jimbo la California, Marekani, kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili katika jimbo hilo.
Akizungumza na Watanzania hao katika Hoteli Embassy iliyoko San Rafael, Rais Kikwete, alisema ni kweli Watanzania wamejiingiza kwa kiasi kikubwa katika ya biashara za ovyo ovyo, ikiwemo dawa za kulevya, lakini serikali yake haitawatetea Watanzania wanaokamatwa.
“Ukikamatwa na dawa za kulevya hatukutetei kwa sababu hata sheria za nchi zetu zinazuia biashara hiyo. Sisi hatuwezi kuendelea kuwa na sifa ya kufanya biashara za ovyo ovyo kiasi hicho.
“Serikali itawatetea Watanzania wanaoishi nchi za nje ikiwa wataonewa. Lakini ukifanya biashara ya dawa za kulevya au kubaka watu hatukutetei kamwe,” alisisitiza Rais Kikwete.
Kuhusu suala la uraia pacha kuwekwa katika Katibu Mpya, Rais Kikwete alisema kuwa katika maoni ya awali suala hilo halikusikika kiasi cha Wajumbe wa Tume ya Katiba kuliweka katika Rasimu ya Katiba.
“Lakini sisi katika CCM tumelizungumza na kuliweka katika mapendekezo yetu mapya tulipokaa kama Baraza la Katiba. Tunataka lizungumzwe. Hatuna hakika kama litawekwa katika rasimu ijayo, lakini tutaendelea kulisemea.
“Kubwa ni kwamba hili ni jambo ambalo halitapata sauti za kutosha kulisemea. Lakini faida zake zinaeleweka hata kama inaelekea kuwa hakuna watu wengi wanaokereketwa na jambo hili kiasi cha kulisema kiasi cha kutosha katika mjadala wa Katiba.”
Hata hivyo, Rais Kikwete aliwashauri Watanzania wanaoishi nchi za nje kuishi kwa amani, kuheshimu sheria na kutojiingiza katika mambo yanayoweza kuwaingiza katika matatizo.
“Lazima muwe raia wema. Mliamua wenyewe kuja kuishi katika nchi hizi. Nchi hizi zina sheria zake. Kama mtaamua kuwa raia wabaya wanaovunja sheria mtaingia katika matatizo – kama wasemavyo Waingereza ‘you will face the music and sometimes that music may not be enjoyable.”
Kuhusu ombi la Watanzania waishio nje  kuruhusiwa kupiga kura, Rais Kikwete alisema serikali yake haina tatizo wala pingamizi na suala hilo ili mradi tu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iwe na uwezo wa kulifanikisha jambo hilo. “Kama wanaweza hakuna kipingamizi. Hatuna matatizo na jambo hili.”



Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru