Thursday 26 September 2013

Agizo la Pinda laanza kutekelezwa



NA SHAABAN MDOE, NGORONGORO
AGIZO la Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kuigawia chakula cha bure jamii ya watu wa Kimasai wapatao 87,000, limeanza kutekelezwa.
Hatua hiyo inayotokana na mamlaka hiyo jana kuanza kugawa kiasi cha tani 700 za mahindi ya chakula kwa jamii hiyo.
Mgawo huo ulianza kutekelezwa ukianzia kata ya Olbalibali, ambapo kaya 1,000 za vitongoji vitano vya tarafa ya Ngorongoro zilipokea chakula hicho kilichogawiwa katika kijiji cha Meshili, huku kaya 508 zikisubiri awamu ijayo.
Vitongoji vilivyopata chakula hicho ni Ngurman, Lorkujita, Nibojijita, Ildonyogoli na Meshili, ambapo kila kaya ilipata debe moja la mahindi bure.
Chakula hicho kilikuwa kimehifadhiwa kwenye maghala, huku kila kaya ikiendelea kusubiri kugawiwa kiasi kingine cha magunia 10.
Akizungumzia mpango huo, Ofisa Ugani wa NCAA, Francis Kone alisema hadi sasa wamenunua magunia 29,000 ya mahindi kutoka wilayani Karatu kwa ajili ya mpango huo wa ili kuwawezesha kuondokana na tatizo la njaa.
Awali, alisema kabla ya agizo hilo, walikuwa na mpango wa kugawa chakula hicho kwa awamu tatu, ya kwanza wakipanga kununua magunia 900, pili magunia 10,000 na tatu magunia 10,000, lakini baada ya agizo hilo, wamelazimika kununuaa magunia yote kwa mkupuo.
Hata hivyo, alisema mamlaka hiyo imedhamiria kutoa magunia mengine 36,000 ya mahindi kwa jamii hiyo, mbali na chakula kilichoahidiwa na Pinda cha magunia matano kwa awamu ya kwanza kwa kila kaya na mengine matano kwa wamu ya pili.
Kone alisema hatua hiyo inatokana na kutambua kuwa hadi sasa chakula kinachogawiwa ni kwa kaya zile zisizo na uwezo kabisa wa kupata chakula.
Mwanakijiji Kanunga Marau aliishukuru serikali kwa chakula hicho, lakini aliiomba kutochelewesha mgawo wa magunia 10 kwa kila kaya ili kuwawezesha wananchi kuwa na uhakika wa chakula wakati wote.
Alisema serikali isiwasahau kwa kuamini chakula kilichotolewa kitakidhi, hasa ikizingatia sheria za uhifadhi katika eneo hilo haziwaruhusu kuendesha hata kilimo cha kujikimu.
Diwani wa Kata hiyo, Metui Ole Shaudo aliipongeza serikali kwa niaba ya wananchi na kusisitiza bado mahitaji ya chakula katika kata yake ni makubwa, hasa ikizingatiwa kaya nyingi ni zile zisizo na uwezo kabisa wa kujipatia chakula.
Aliiomba serikali kutimiza ahadi ya ugawaji wa magunia 10 kwa awamu mbili kwa kila kaya ili kuwajengea imani na kuwafanya waendelee kuwa wahifadhi waaminifu wa hifadhi hiyo na wanyamapori waliopo.
Mwanzoni mwa juma lililopita, Waziri Mkuu Pinda akiwa katika tarafa hiyo aliwaahidi wananchi hao kuwa serikali itabeba jukumu la kuwapatiwa chakula wananchi hao kila mwaka wakati ombi lao la kutaka waruhusiwe kuendesha kilimo likifanyiwa kazi.
Ends.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru