Saturday 14 September 2013

Padri amwagiwa tindikali Zanzibar


NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
PADRI wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mpendae, Zanzibar, Anselmo Wan'gamba, amemwagiwa tindikali usoni na watu wasiojulikana.
Tukio hilo lilitokea jana, saa 10.30 jioni, eneo la Mlandege wakati akitoka kupata huduma ya mawasiliano ya internet.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba, wanaendelea na uchunguzi wa kina ambao tayari umeanza.
Padri Mwang'amba ni Mkuu wa Kituo cha Malezi cha Vijana kilichopo Cheju, Mkoa wa Kusini Unguja, ambacho kinatunza vijana kwa ajili ya kuwapatia mafunzo mbalimbali.
Mkadam alisema walipokea taarifa hiyo na wanafanya uchunguzi ili kufahamu mtandao wa watu wanaojihusisha na uhalifu huo.
Kwa upande wake, Daktari wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, ambaye alimpokea padri huyo hospitalini hapo, Abdalla Haidari, alisema kiongizi huyo wa dini ameumua usoni na kifuani.
Alisema padri huyo amejeruhiwa na kwamba baada ya kumfanyia uchunguzi waligundua kuwa amemwagiwa tindikali.
Dk. Haidari alisema katika maelezo ya padri huyo, alishambuliwa na watu ambao hakuwafahamu wakati akitokea Sunshine, Mlandege.
Alisema wakati anatoka kupata huduma hiyo alimwagiwa maji aliyohisi tindikali na kukimbilia hospitalini hapo.
Naye mfanyakazi wa internet hiyo aliyejulikana kwa jina moja la Salama, alikiri padri huyo kufika na kupata huduma hiyo na kuondoka, lakini alishangaa kumuona akirudi huku akilalamika kufanyiwa kitendo hicho.
Mei 23, mwaka huu, Sheha wa Shehia ya Tomondo, Wilaya ya Magharibi Unguja, Mohammed Omar Said (65), alimwagiwa tindikali na mtu asiyejulikana alipokuwa akichota maji nje ya nyumba yake majira ya saa 2:45, usiku.
Tukio lingine ni lile la Agosti 9, mwaka huu, ambalo lilidaiwa kufanywa na watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki maarufu kama Vespa, mjini Zanzibar, ambapo raia wawili wa Uingereza, Kate Gee (18) na Kristie Trup (18) walimwagiwa tindikali.
Tukio hilo lilitokea lilitokea saa moja usiku wakati raia hao walipokuwa wakitoka kunywa kahawa katika Baraza la Jaws Corener, mjini humo.
Pia, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Fadhili Soraga, alifanyiwa unyama huo Desemba, mwaka jana na mtu asiyefahamika wakati akifanya mazoezi.



Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru