MCHANGO wa sekta ya madini katika pato la Taifa umekuwa kutoka asilimia 2.9 mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 3.5 mwaka 2012.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, alipokuwa akijibu swali la Sylvester Mabumba (Dole- CCM).
Katika swali lake, Mabumba alitaka kujua ni kwa kiasi gani sekta ya madini imechangia uchumi wa taifa katika kipindi cha miaka minane iliyopita.
Masele, alisema katika kipindi hicho, mchango wa sekta hiyo ya madini kwa mauzo ya nje ya nchi umekuwa kwa wastani wa asilimia 40.3.
Naibu Waziri, huyo alisema katika kipindi cha miaka minane iliyopita kuanzia mwaka 2005 hadi 2012, kuna ongezeko kubwa la mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa hususani pato la taifa na mchango wa mauzo ya nje.
Alisema mwaka 2005 hadi 2012, serikali iliingia mkataba mmoja wa uendelezaji wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi Wilayani Kahama, mwaka 2007.
Masele, alisema mgodi huo unamilikiwa na kampuni ya Pangea Mineral Limited, kampuni tanzu ya African Barrick Gold (ABG).
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010, mikataba ya uendelezaji wa miradi ya madini huingiwa endapo mmiliki ataomba kuingia mkataba na serikali.
Na iwapo gharama za uwekezaji katika mradi husika hazipungui dola za kimarekani milioni 100, (Sh. bilioni 1.6).
Alisema serikali kwa sasa inafanya jitihada kuhakikisha wafanyakazi wazawa walioko katika migodi mikubwa, wanalipwa kulingana na taaluma zao sambamba na watumishi wageni katika vyeo vinavyofanana.
Naibu Waziri huyo, alilieleza Bunge kuwa serikali inaendelea kuyasimamia na kuyalinda maslahi ya watumishi wazalendo.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2005 hadi 2012, kumekuwepo na ongezeko la ajira kupitia uwekezaji unaofanywa katika sekta ya madini.
Alisema katika kipindi hicho ajira za wazawa katika migodi mikubwa imeongezeka kutoka 2,077 mwaka 2005 hadi 13,000 mwaka 2012.
Tuesday, 3 September 2013
Sekta ya madini yapaa uchangiaji pato la taifa
08:58
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru