NA MWANDISHI WETU, MBEYA
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Mbeya, imeongeza uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 32,000 kwa siku hadi mita za ujazo 50,000.
Hali hiyo imesababisha upatikanaji wa maji ya kutosha ambapo asilimia 96 ya wananchi wanapata maji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Injinia Simeon Shauri, aliyasema hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa, Abbas Kandoro, wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya mamlaka hiyo.
Shauri alisema mamlaka imeweza kujiendesha kibiashara kwa kujitegemea na uwezo huo umetokana na kukamilika kwa miradi ya maji na usafi wa mazingira ya awamu ya kwanza na ya pili.
ìWateja wa majisafi wameongezeka kutoka 24,388 hadi wateja 34,242, na kwa upande wa majitaka wameongezeka kutoka wateja 379 hadi 1,261 kwa sasa,î alisema.
Alisema huduma imeboreshwa kutoka wastani wa saa 21 kwa siku hadi saa 23 kwa siku, ambapo asilimia 78 ya wateja wanapata maji saa 24 kwa siku.
Mkurugenzi huyo alisema mahitaji halisi ya maji mjini hapa kwa sasa ni wastani wa mita za ujazo 42,000 kwa siku, hata hivyo, wakati wa kiangazi hupanda hadi mita za ujazo 46,000 kwa siku na hiyo hutokea Agosti, Septemba na Oktoba.
Alisema mamlaka inavyo jumla ya vyanzo 13 vya maji, ambavyo kwa jumla hutoa mita za ujazo 50,000 kwa siku, huku vyanzo hivyo vikiwa na mitambo 10 ya kusafisha na kutibu maji.
Kwa mujibu wa Injinia Shauri, mitambo hiyo ipo katika maeneo ya Swaya, Imeta, Sisimba, Lunji, Mwatezi, Iduda, Nzovwe, Iyela, Nsalaga na Nelotia.
Naye, Kandoro alisema mamlaka hiyo imeendelea kujitegemea na kuwapongeza wajumbe wa bodi iliyomaliza muda wake chini ya Dk. Grant Mwakatundu kwa kuweza kuisaidia mamlaka kuweza kutoa huduma stahili kwa wakazi wa jijini hapa.
Kandoro aliwataka wajumbe waliomaliza muda wao kushirikiana na bodi mpya ambayo itaongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Atuganile Ngwala, kutokana na kuwa na uzoefu.
Tuesday, 17 September 2013
Wananchi asilimia 96 wapata majisafi
08:06
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru