Wednesday 18 September 2013

Pinda ahidi serikali kuzidi kushirikisha ngazi za chini


Na Jesca Kileo
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema serikali itaendelea kushirikiana na wabia wa maendeleo ili kuimarisha utawala bora na hatimaye kusaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika ngazi za chini.
Pia, ameagiza watendaji wa ngazi za chini kutoa taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi badala ya kuzificha, kwani hatua hiyo itasaidia kuongeza uwazi na kujenga imani kwa wananchi wanaowaongoza.
Alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua maadhimisho ya Siku ya Soko la SULGO yaliyoandaliwa na TAMISEMI kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Ujerumani (GZI).
Alisema maonyesho hayo yamelenga kujenga uwezo kwenye serikali za mitaa ili waweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi kwa kuwapatia mafunzo yatakayowawezesha kuwa na vyanzo vya fedha, kuwekewa mifumo ya kupata fedha hizo, kuwezeshwa kusimamia matumizi ya fedha zao na kujengewa ushirikishwaji wa wananchi kuanzia ngazi ya chini hadi taifa.
ìSerikali za Mitaa ndiyo nyenzo kuu ya serikali katika utekelezaji wa shughuli za serikali, na fedha nyingi zinapelekwa huko ambako miradi ya maendeleo iko. Utaona kuna fedha ni jambo moja lakini kuweza kusimamia matumizi ya zile fedha ni jambo lingine kwa hiyo wametoa mafunzo kwa watendaji wa vijiji na kata juu ya suala hili,î alisema.
Akizungumza na waadishi wa habari baada ya kukagua maonyesho hayo, Waziri Mkuu Pinda, alisema amefurahi kuona katika ngazi ya chini kabisa wananchi wamejengewa uwezo wa kutambua jinsi sheria ndogo zinavyotungwa.
Aliishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia GIZ ambayo imetoa Euro milioni 9.8 kwa ajili ya kusaidia mradi huo unaotekelezwa kwa majaribio kwenye wilaya za mikoa ya Tanga na Mtwara. Wilaya hizo ni Mtwara, Nanyumbu, Tandahimba na Masasi kwa mkoa wa Mtwara wakati mkoani Tanga unatekelezwa katika wilaya za Handeni, Muheza, Jiji la Tanga na wilaya ya Tanga.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu, kufungua maonyesho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Hawa Ghasia, alisema soko la SULGO ni dhana ya ushirikishwaji wa wananchi katika kutoa maamuzi kuanzia ngazi ya chini, ngazi ya wilaya na hatimaye ngazi ya taifa au serikali kuu.
Alisema dhana hiyo, imekuwa ikiendeshwa chini ya Mpango wa Serikali wa Maboresho ya Serikali za Mitaa (LGRP). Alisema mradi huo wa Soko la SULGO ulianza Januari 2008 na unatarajiwa kukamilika Septemba mwakani.
Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano kutoka Ubalozi wa Ujerumani, Claudia Imwolde-Kraemer, alisema mradi huo umelenga kuimarisha utendaji wa serikali za mitaa kwa kufuatilia ukusanyaji wa mapato na kuweka mifumo ya uwajibikaji kwenye masuala ya fedha.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru