Wednesday 25 September 2013

Maiti ya dawa za kulevya Mazito yafichuka


Na Mwandishi Wetu
SIRI ya kifo cha mfanyabiashara Rajabu Rajabu aliyefariki dunia, baada ya kumeza pipi 33 za dawa za kulevya zenye thamani ya mamilioni ya fedha, imefichuka.
Marehemu Rajabu mkazi wa Ilala, Dar es Salaam, alifariki dunia juzi, baada ya dawa hizo aina ya Heroine kumpasukia tumboni.
Kufuatia tukio hilo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inawashikilia asri Rajabu ‘Robot’ na Mwanaisha Kapama, wakazi wa Kigogo Luhanga, wakiwa na maiti ya mfanyabiashara huyo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umeibua siri nzito baada ya kubaini kuwa kabla ya umauti kumfika, marehemu aliondoka na dawa hizo kutoka Dar es Salaam kwenda Msumbiji.
Habari za uhakika kutoka chanzo chetu cha habari zinadai kuwa, marehemu alifikia katika nyumba ya kulala wageni mkoani Mtwara kwa ajili ya kuangalia hali ya usalama katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji.
Chanzo hicho kilidai marehemu alikaa katika nyumba hiyo kwa muda wa siku tatu na kwamba, afya yake ilibadilika ghafla na kushindwa kutoka nje ya nyumba hiyo.
“Huyo marehemu alikodi chumba kwenye ‘Guest’ moja ili kuangalia hali ya usalama mpakani ili aweze kuendelea na safari yake.
“Lakini hafla hali yake ilibadilika na kukaa ndani siku nzima bila kutoka nje, hivyo mhudumu wa ile nyumba alilazimika kuingia ndani ya chumba kumuangalia.
“Hata hivyo, mhudumu alimuona akiwa katika hali mbaya na ndipo alipomwuliza wenyeji wake na alimpa namba ya simu ya kaka yake anayeishi Ilala,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo chetu hicho, baada ya kaka wa marehemu kupewa taarifa ya mdogo wake kuumwa, walilazimika kwenda Mtwara na mke wa marehemu.
Kilisema kaka wa marehemu aliondoka na gari aina ya Toyota Land Cruiser VX na kwamba, marehemu alikuwa amepakatwa na mke kwenye kiti cha nyuma ya gari hiyo.
Chanzo hicho kilisema kuwa, wakati wanarudi walipofika maeneo ya TAZARA, Dar es Salaam, Rajabu alifariki dunia na dereva wa gari hilo aliteremka kwa muda.
“Huyu jamaa alifia pale TAZARA na alikuwa amepakatwa na mkewe… baada ya kubaini amefariki ilibidi dereva ateremke kidogo kuhakikisha kama ni kweli.
“Wananchi baada ya kumwona dereva ameteremka kwenye gari na kuja nyuma, ndipo walipoitilia shaka na kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Buguruni, ambapo polisi walianza kufuatilia ile gari,” kilieleza chanzo hicho.
Kilisema marehemu alipelekwa maeneo ya Tabata Mawenzi na muda mfupi baada ya kuingizwa kwenye nyumba hiyo, askari walifika na ndipo alipobainika alikuwa amemeza dawa.
Chanzo chetu hicho cha habari kilisema kuwa, marehemu anajihusisha na biashara hiyo kwa muda mrefu kwenye nchi mbalimbali, ikiwemo Msumbiji.
Juzi, gazeti hili liliripoti habari ya kufariki kwa mfanyabiashara huyo, baada ya kuwa amemeza pipi 33 za dawa za kulevya, ambazo hata hivyo, zilimpasukia tumboni.
Siku moja baada ya kuripoti habari hiyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alisema wanawashikilia Rajabu na Mwanaisha wakiwa na maiti ya marehemu.
Kova alisema taarifa zinaonyesha marehemu alikuwa mhalifu mzoefu wa usafirishaji wa dawa za kulevya, na kwamba kabla ya kurudi nchini alikuwa anatumikia kifungo barani Asia.
Alisema baada ya polisi kupata taarifa ya tukio hilo, walikwenda nyumbani kwa Rajabu maeneo ya Tabata na kumhoji, ambapo waligundua uwepo wa maiti sebuleni ikiwa imelazwa chali kwenye godoro.
Kova alisema Rajabu ndiye mmiliki wa chumba ilimokutwa maiti na uchunguzi unaonyesha marehemu alifika kutoka Mtwara, na juzi na kabla ya kufa mfanyabiashara huyo, alikwenda bafuni kuoga na alirudi katika chumba hicho na ndipo alipokutwa na umauti.
Kamishna huyo, alisema mazingira ya kifo hicho ndiyo yaliyosababisha polisi kupata taarifa na walipofika eneo la tukio waliuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa uchunguzi.
Hata hivyo, alisema uchunguzi unaendelea
ili kubaini mtandao wa usafirishaji wa dawa hizo ambao umehusisha marehemu na watakaokamatwa watachukuliwa hatua za kisheria.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru