Tuesday, 3 September 2013

Mahakama kulichukulia Jamhuri hatua


NA MWANDISHI WETU
JAJI Kiongozi Fakihi Jundu, amesema mahakama inafikiria hatua za kulichukulia gazeti la Jamhuri kutokana na kukiuka maadili kwa kuidhalilisha kwa kutaja majina ya majaji na mahakimu kuwa wanahusika kuwasaidia wauza ‘unga’.
Pia, amewaasa waandishi kuwa makini na kuzingatia maadili ya uandishi wa habari za mahakama, wanapoandika habari za kesi zinazoendelea mahakamani au zilizokwishwa.
Jaji Kiongozi aliyasema hayo jana mjini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu habari iliyochapishwa na gazeti la Jamhuri toleo la Agosti 27 hadi Septemba 2, mwaka huu, iliyokuwa na kichwa cha habari kisomekacho: ‘Majaji wanaolinda wauza ‘unga’ wabainika’.
Alisema ndani ya habari hiyo imetaja majina ya majaji na mahakimu na kesi zinazoendelea kusikilizwa, na kuongeza kuwa habari hiyo imewasononesha, kwani ni tuhuma nzito na zenye lengo la kuichafua mahakama ili wananchi wakose imani nayo.
“Tuhuma hizo kwa uzito wake ilimpasa mwandishi wa gazeti husika, kukutana na uongozi wa mahakama ili aweze kupata taarifa mbalimbali alizoziandika.
“Uongozi wa mahakama una taratibu zake za namna ya kutoa taarifa, iwapo mtu yoyote anahitaji kuhusu suala fulani lilivyoendeshwa au katika kupata taarifa fulani zenye manufaa kwa nchi yetu,” alisema.
Alisema kumekuwa na taarifa nyingi zinazozungumzwa dhidi ya mahakama ambazo si za kweli na hata waandishi wameshindwa kwenda kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwa uongozi wa mahakama.
“Madhara ya uandishi wa namna hii, usiofuata mila na miiko ya uandishi wa masuala ya kimahakama zaidi kuhusu masuala ya namna ya uendeshaji wa kesi, uamuzi uliotolewa, muonekano hasi, yanayoonekana katika rangi yake sawia, hauna nia njema katika ustawi wa amani ya nchi ambayo inaendeshwa kwa misingi ya utawala wa sheria,” alisema.
Alisema katika habari hiyo imetaja majina ya majaji wakiwatuhumu kwa kutoa dhamana kwa washitakiwa kinyume cha sheria na wengine kuwaachia watuhumiwa.
Akifafanua zaidi, alisema miongoni mwa kesi zilizotajwa ipo ambayo mshitakiwa aliachiwa kutokana na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi ambapo mahakama inakuwa haiwezi kukataa.
Jaji Kiongozi alizitaja kesi zilizolalamikiwa kuwa kesi namba 47 ya mwaka 2011 ya Jamhuri dhidi ya Fredy Chonde, ambapo alisema ipo Mahakama ya Rufani, na kwamba inaendelea kwa ajili ya pingamizi la dhamana na inaendelea Mahakama Kuu, hivyo kuizungumzia na kuitolea mfano katika magazeti haifai kisheria.
Kesi nyingine ni P1 namba 26 ya mwaka 2011, iliyokuwa mbele ya Jaji Dk. Fauz Twaib, ambapo inadaiwa mahakama ilimuachia mshitakiwa.
“Kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama ni kuwa si kweli Jaji Dk. Fauz alimwachia mshitakiwa kwa matakwa yake binafsi au kutumia kivuli cha mahakama, bali upande wa mashitaka ulileta maombi ya kuondoa kesi,” alisema.
Akizungumzia kuhusu vita dhidi ya dawa za kulevya, Jaji Kiongozi alisema ili kufaulu katika mapambano dhidi ya hilo, unahitajika ushirikiano wa vyombo husika.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru