Wednesday 11 September 2013

Kinana atoa somo kwa wamiliki migodi


NA SULEIMAN JONGO, KAHAMA  
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amewataka wawekezaji nchini hasa wa migodi ya madini, kutoa kipaumbele kwa jamii inayowazunguka pindi wanapotaka kuchangia miradi ya maendeleo.
Kinana aliyasema hayo juzi wakati akikagua ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Mwendakulima, wilaya ya Kahama, Shinyanga, akiwa katika ziara ya kikazi kwenye mikoa mitatu ya kanda ya ziwa.
Alisema ili kuhakikisha wananchi hasa walio kwenye maeneo ya uwekezaji wa miradi mbalimbali, wanapaswa kuacha kiasi kikubwa cha fedha walizozitenga kwa ajili ya kushiriki maendeleo ya taifa. 
“Kwa mfano hapa Kahama, wapo wawekezaji wanaochimba madini, ni vyema wakashiriki kikamilifu kwa kuacha asilimia 90 ya bajeti yao ya kuchangia miradi ya maendeleo badala ya kupeleka katika maeneo mengine kwa ajili ya kuwafurahisha viongozi,” alisema Kinana.   
Kwa mujibu wa Kinana, endapo wawekezaji watazingatia hilo, wataondoa mgogoro kati yao na wananchi kwa kuwa wataona manufaa ya moja kwa moja yanayotakana na rasilimali zao.     
Kwa upande wake, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, aliwataka wananchi kuwa karibu na mchakato wa katiba mpya ili kuwabaini watu wanaotaka kupenyeza maslahi yao binafsi kwa lengo la kuuharibu mchakato huo.   
Nape, alisema wananchi wana nafasi kubwa katika kuhakikisha mchakato huo unafanikiwa na hatimaye kupatikana kwa katiba ya Watanzania wote. 
“Fuatilieni mchakato wa katiba mpya kwa karibu, kwa kuwa wapo baadhi ya watu hasa kutoka vyama vya upinzani kikiwemo CHADEMA, ambao kwa makusudi wanataka kuharibu mchakato huu kwa maslahi wanayoyajua wao. 
Nape na Kinana, wako kwenye ziara ya wiki tatu katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara, ambako watatembelea wilaya zote kuhamasisha maendeleo ya jamii.  

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru