Wednesday 18 September 2013

CHADEMA yadaiwa kipoteza mwelekeo


Na Mwandishi Wetu, Morogoro
NAIBU Katibu Mkuu wa Jumuia ya Wazazi (Bara) Glorious Luoga, amekiponda CHADEMA kwa madai kuwa kimepoteza mwelekeo kisiasa kutokana na kuendesha sera za chuki na matusi dhidi ya viongozi wa CCM.
Alisema sera za namna hiyo kamwe hazikubaliki na hazipaswi kupewa nafasi katika jamii kwa kuwa zinaashiria uvunjifu wa amani na utulivu uliopo nchini.
Luoga alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliyofanyika Gairo mkoani Morogoro.
Alisema CHADEMA kimeshindwa kufanya shughuli zake kama chama cha kisiasa kwa kunadi sera zake na badala yake viongozi wake wamekuwa wakipanda katika majukwaa na kuanza kuwashambulia kwa matusi viongozi wa CCM.
Hata hivyo, Luoga aliwafananisha viongozi hao wa CHADEMA na watoto waliokuwa wakiishi maisha ya tabu na njaa kali kwa kipindi kirefu, lakini baada ya kupewa chakula na kushiba wakasahau shida iliyowapata na kuanza kutukana wazazi wao waliowapa chakula.
ìHakuna asiyejua kama CHADEMA sasa wamelewa shibe baada ya kuonewa huruma na kupata viti vichache vya madiwani na wabunge.
ìKabla ya kupata viti hivyo kimekuwa kikiendesha sera za kiustaraabu, lakini sasa kimejijengea utamaduni wa kulazimisha kutumia lugha ya matusi dhidi wa CCM waliowafundisha siasa na mpaka kufikia hapo kilipo,î alisema Luoga.
Alisema CCM haitishiki na siasa hizo uchwara na badala yake itazidi kujikita kuimarisha Chama hicho na kutekeleza Ilani yake ya uchaguzi kwa kuwaletea maendeleo wananchi wake bila kujali itikadi za kisiasa, rangi, kabila wala dini.
Luoga aliwataka wananchi wa Gairo wasikubali kufanya makosa kwa mara nyingine katika uchaguzi mkuu ujao kwa kuchagua wagombea wa vyama vya upinzani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru