Wednesday, 4 September 2013

Hakuna maendeleo bila kukopa -Dk. Bilal


Na Rachel Kyala
WATANZANIA wametakiwa kujenga tabia ya kulipa mikopo wanayokopa ili kuleta maendeleo endelevu.
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, aliyasema hayo jana kwenye hafla ya ufunguzi wa benki ya United Bank Limited (UBL), jijini Dar es Salaam.
Alisema hakuna maendeleo yoyote makubwa yanayoweza kufikiwa bila ya mikopo, hivyo ni vyema wananchi wakatumia vyema fursa hizo kwa manufaa yao na wengine.
“UBL ni benki kubwa duniani na ina matawi katika mabara ya Amerika, Ulaya na Asia. Hivyo ni jambo la kujivunia kuanzishwa kwa benki hii hapa Tanzania, kwani ndilo tawi la kwanza kufunguliwa barani Afrika,” alisema Dk. Bilal.
Makamu wa Rais aliutaka uongozi wa benki hiyo kuweka gharama nafuu kwenye huduma zake, hususan zile za kufungua akaunti, kuweka na kuchukua fedha pamoja na riba nafuu kwa mikopo wanayotoa ili kuwawezesha wananchi wengi kupata huduma hiyo muhimu.
Pia, aliishauri UBL kuunganisha huduma zake na mitandao mbalimbali ya simu ili kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi, hasa wenye kipato cha chini na wale wanaoishi nje ya miji.
Aliitaka benki hiyo kuingia ubia na kampuni zinazouza vifaa vya kilimo ili kushirikiana nazo na kuwezesha kuwakopesha wananchi vifaa hivyo.
Alisema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi, juu ya gharama kubwa za kupanga nyumba ambapo serikali sasa ipo kwenye mchakato wa kukopa fedha Benki ya Dunia, zitazokopeshwa kwa benki ili kutoa mikopo nafuu ya nyumba kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa UBL, Atif Bokhari, alisema tayari wametoa ajira kwa Watanzania 20, na kwamba wanatarajia kufungua matawi sehemu mbalimbali nchini na kuongeza idadi ya watumishi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru