Tuesday 3 September 2013

Kisiwa cha Saanane sasa hifadhi ya taifa


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
KISIWA cha Saanane kilichopo ndani ya Ziwa Victoria, kimetangazwa kupandishwa hadhi kutoka pori la akiba kuwa hifadhi ya taifa.
Hatua hiyo, imekuja baada ya Oktoba, mwaka jana, bunge kupitisha azimio la kuruhusu kisiwa hicho kupandishwa hadhi kutoka pori la akiba hadi hifadhi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Paschal Shelutete, alisema kisiwa hicho kimepandishwa hadhi kuwa hifadhi kwa mujibu wa tangazo la serikali namba 227.
Shelutete alisema pamoja na kuwa hifadhi, Kisiwa cha Saanane kimeongezwa ukubwa hadi kufikia kilomita za mraba 2.18, likijumuisha visiwa vya Chankende na eneo lote la maji ya Ziwa Victoria linalozunuka kisiwa hicho.
“Kuanzishwa kwa hifadhi hii kutasaidia kutunza bioanuwai, hifadhi, mazalia na makuzio ya samaki katika la Ziwa Victoria, ambayo ilikuwa ikitishiwa na vitendo vya uvuvi haramu unaoangamiza hadi mayai ya samaki,” alisema.
Pia, alisema uamuzi huo utaongeza spishi mbalimbali za wanyamapori na hivyo kuongeza utalii wa mjini kutokana na hifadhi hiyo kuwa katikati ya jiji la Mwanza.
Awali, kKisiwa hicho cha Saanane kilikuwa bustani ya wanyama kabla ya kupandishwa hadhi kuwa pori la akiba na baadaye kuwekwa chini ya uangalizi wa TANAPA.
Jumla ya hifadhi za taifa sasa zitafikia 16. Hifadhi zingine ni Serengeti, Ziwa Manyara, Tarangire, Arusha, Mikumi, Kilimanjaro, Gombe, Kisiwa cha Rubondo na Milima ya Mahale, Mkomazi, Milima ya Udzungwa, Ruaha na Kitulo.
Wakati kisiwa cha Saanane kikipandishwa hadi kuwa hifadhi, serikali imetangaza kuongeza eneo la hifadhi ya taifa la Gombe kwa umbali wa kilomita za mraba 33.74 hadi kilomita za mraba 56.
Tangazo la serikali namba 228 limesema uamuzi huo wa kuongeza eneo la hifadhi ya Gombe, umezingatia azimio la bunge la kurekebisha mipaka ya hifadhi hiyo kwa kujumuisha eneo la ufukwe wa maji ya Ziwa Tanganyika na eneo la ukanda wa maji ya ziwa hilo.
Shelutete alisema ongezeko la eneo la ukanda wa maji katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe, kutaongeza wigo wa shughuli za utalii katika hifadhi, ikiwemo kuogelea, utalii wa boti, mitumbwi na uvuvi wa kitalii.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru