Wednesday 4 September 2013

Mwenge Dar kuzindua miradi ya sh. bilioni 23


Na Mohammed Issa
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Juma Ali Simai, amesema Mwenge utaendelea kuenziwa na wanaoukataa wana ajenda binafsi, huku ikielezwa jijini Dar utazindua miradi ya sh. bilioni 23.2.
Amesema Mwenge ni hazina itakayoendelea kuenziwa na kutunzwa kwa manufaa ya taifa na wananchi wake.
Simai alisema hayo jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, katika mapokezi ya mbio za Mwenge ulioanza kukimbizwa mkoani humo.
Mbali na hilo, Simai aliwataka vijana kuacha matumizi ya dawa za kulevya, kwani yanaleta madhara makubwa katika jamii na taifa kwa jumla.
Mwenge huo ulikabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadiki na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mtwantum Mahiza.
Katika makabidhiano hayo, Simai alisema Mwenge utaendelea kuenziwa na wanaoukataa wana sababu zao binafsi.
ìTusikubali kuwapa nafasi wanaobeza mbio za Mwenge wa UhuruÖwatakuwa wanaukataa kwa sababu zao binafsi, lakini tuwapuuzeni,î alisisitiza.
Alisema vijana ni nguvu ya taifa, hivyo wanapaswa kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya ambazo zinawasababishia madhara makubwa maishani.
Kwa upande wake, Sadiki alisema mkoa umejiandaa vya kutosha kuupokea Mwenge huo ambao utakimbizwa kwenye wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke na kuzindua miradi 26 ya maendeleo yenye thamani ya sh. bilioni 23.2.
Alisema katika wilaya ya Kinondoni, utazindua miradi sita ya maendeleo yenye thamani ya sh. bilioni 2.8 na utalala katika Shule ya Msingi Bunju A.
Sadiki alisema, leo Mwenge utakimbizwa katika wilaya ya Ilala na utazindua miradi tisa yenye thamani ya sh. bilioni 1.3.
Alisema kesho utakimbizwa kwenye wilaya ya Temeke na utazindua miradi 11 yenye thamani ya sh. bilioni 19.11.
Mkuu huyo wa mkoa alisema ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni mahsusi wenye lengo la kuleta umoja na mshikamano ambao unasema: ‘Watanzania ni wamoja, tusigawanywe kwa misingi ya tofauti zetu na dini, itikadi, rangi na rasilimali’.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru