Tuesday, 10 September 2013

Rais amuumbua ofisa mifugo



NA PETER KATULANDA,MWANZA
RAIS Jakaya Kikwete, amemshukia Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Kwimba, mkoani hapa na kumtaja kuwa kikwazo cha maendeleo ya mifugo wilayani humo.
Alidai kuwa anakwamisha mpango wa uzalishaji ng’ombe kwa njia ya kisasa ya uhamilishaji mbegu (AI).
Aliyasema hayo juzi wakati alipopokea taarifa ya Mkuu wa wilaya hiyo, Selemani Mzee.
Rais Kikwete, alisema njia ya kuzalisha ng’ombe wa kisasa kwa kupandisha madume inayotumiwa wilayani humo, haiwezi kuleta mafanikio ya haraka.
Kwa mujibu wa Rais, maendeleo hayo yatachukua miaka 100, kutokana na Ofisa huyo, Eliakim Ole Wavia, na wasaidizi wake, kushindwa kutumia njia za kisasa.
“Hebu kwanza…mmesema mnazo ng’ombe 390,000, sasa kama mnatumia njia ya kupandikiza mbegu kwa kutumia madume 12 kwa idadi hiyo ya ng’ombe, lengo la kumaliza mifugo 390,000 si litakamilika miaka 100, kwa nini hamtumii njia ya kupandikiza mbegu,” alihoji Rais Kikwete.
Awali, Wavia, alisema walifikia uamuzi huo baada ya kupandisha mbegu 38 na kupata mimba tatu, hivyo kuamua kutumia njia ya kupandisha madume.
Alisema walianza na madume 12, lakini katika mkakati mpya wamepanga kuongeza madume 32, kwa wastani wa dume moja kwa majike 32.
Maelezo hayo, yalimshangaza Rais Kikwete ambapo alisema ofisa huyo ni kikwazo cha kufanikiwa kwa mpango wa uhamilishaji, iwapo ataendelea na mpango wake huo.
“Wewe bwana mifugo unanishangaza sana, mbona mimi shambani kwangu ninapandikiza kwa njia ya mbegu na mafanikio nayaona,  ilikuwaje ninyi mbegu 38 mpate mimba tatu, basi wewe na mnaopandisha si wataalamu,” alisema Rais Kikwete.
Kutokana na hilo, Rais Kikwete alilazimika kumpa darasa la uhamilishaji akieleza anavyofanya yeye katika shamba lake huo Chalinze mkoani Pwani.
Alisema kwa watalaamu wazuri, kazi ya kwanza huwa ni kuchagua dume bora la mbegu na kisha kulidanganya ili kupata mbegu.
Alisema mbegu zinapopatikana, jike huchomwa sindamo maalumu ambayo katika kipindi cha saa 72, hupevusha yai na ndipo mbegu hupandishwa, mpango ambao ni wa uhakika kwa asilimia 100.
Alisema hata ikikwama, mafanikio yake ni asilimia 80 kiasi ambacho ni kikubwa kuliko cha kutumia madume.

1 comments:

  1. Hiyo njia ya kupiga sindano ili ng'ombe aingie kwenye joto (heat synchronization)ni aghali mno kwa mkulima wa kawaida, na baada ya hapo inabidi alipie tena na ng'ombe wake kupandishwa ndio maana wafugaji wengi wanashindwa, ni rahisi kukodi dume la kupandishia

    ReplyDelete