Tuesday, 17 September 2013

Chagua jibu sahihi katika hisabati yamkera waziri


NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema ufaulu wa somo la hisabati katika shule za msingi na sekondari nchini hauridhishi.
Amesema mustakabali wa taifa unawataka wadau wote kuunganisha nguvu ili kukabiliana kikamilifu na changamoto hiyo.
Dk. Mwakyembe alitoa rai hiyo wakati wa ufunguzi wa semina ya hisabati na mkutano wa kitaifa wa mwaka wa 48 wa Chama cha Hisabati Tanzania, unaofanyika Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU), mjini hapa.
Alisema matokeo ya somo la hisabati kitaifa ni changamoto kubwa, na kwamba serikali itaendelea kukiunga mkono chama hicho katika kuhakikisha kinafanikiwa kutimiza malengo yake ya kuinua somo hilo nchini.
Aidha, waziri alisema serikali itahakikisha kuwa walimu wengi zaidi wanahudhuria mikutano ya chama hicho na siyo kama ilivyo sasa, ambapo mahudhurio hayaridhishi.
ìHuu ndio mzaha uliopo katika utendaji wetu wa kaziÖ ni lazima walimu wote waliokuwa wamepewa taarifa za semina na mkutano huu kisha hawajahudhuria wajieleze walikuwa wapi. Hatuwezi kuendelea kuifumbia macho hali hii,î alisisitiza.
Alisema  atahakikisha analifikisha suala hilo kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, kuhusu hali hiyo ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya wahusika.
îImekuwa ëbusiness as usuallyí na hili nawaahidi kuwa nitalifikisha mbele zaidi kwa waziri husika, ili kila aliyepewa mwaliko, lakini hajafika atueleze alikuwa wapi, kama alikuwa amempeleka mkewe kusuka, atueleze,” alisema.
Waziri alisema anaungana na chama hicho kupinga mfumo wa kuchagua jibu sahihi katika mitihani ya hisabati kwa shule za msingi, kwani haiwajengi wanafunzi kufikiri.
Alikiri ni vyema mfumo huo uachwe kutumiwa na wanafunzi wa shule za msingi, bali uendelee kwa shule za sekondari ili watoto wa shule za msingi wajifunze somo hilo kwa ufasaha zaidi na siyo kupitia mfumo huo wa kuchagua.
Dk. Mwakyembe alisema kwa hali ilivyo, bado siyo sahihi kwa mfumo huo kutumika kwa shule za msingi, hivyo ni lazima kwanza mtoto aanze kujengewa msingi imara wa somo hilo tangu akiwa shule ya msingi.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru