Wednesday 18 September 2013

Wakulima wa pamba waishukia CHADEMA

na mwandishi wetu, Simiyu
HATUA ya CHADEMA kumshambulia Balozi wa China nchini, Dk. Lu Youqing kwa kupanda jukwaani kuelezea mambo mazuri ambayo serikali ya nchi hiyo imepanga kuwafanyia wakazi wa Shinyanga, hususan wakulima wa pamba, imewakera wananchi na kuwaonya viongozi wa chama hicho kuacha kuweweseka.
Wamesema siasa za chuki na hila zinazofanywa na viongozi wa CHADEMA dhidi ya Balozi Dk. Lu zimewakera, na kwamba hatua za kuanzisha viwanda na kuokoa zao la pamba zinazofanywa na serikali ya China zinapaswa kuungwa mkono na yeyote, na mwenye kupinga hana mapenzi mema na wakulima nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wakulima hao walimweleza Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kuwa, wamechukizwa na hila na ghilba zinazoendeshwa na CHADEMA kwa kushirikiana na vyama vingine kupinga hatua za China katika kuwakomboa Watanzania kwa kuwaletea maendeleo ya kweli.
‘’Kwa muda mrefu wakulima wa pamba tunakabiliwa na changamoto nyingi, sasa wenzetu ambao ni marafiki wa kweli wameamua kuchukua hatua za kutusaidia, lakini wanasiasa wachache kwa maslahi yao wameamua kupotosha ukweli.
“Kumshambulia balozi kwa kupanda jukwaani kueleza mambo ya maendeleo wanayotufanyia si uungwana na inaonyesha wazi namna ambavyo viongozi wa CHADEMA walibvyo wanafiki na hawana mapenzi ya dhati na Watanzania, hususan wa Kanda ya Ziwa ambao wanategemea zao hili kujiletea maendeleo,’’ alisema Shija Mabula kwa niaba ya wananchi wenzake.
Alisema viongozi wa CHADEMA, akiwemo Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa, wamekuwa vinara wa kuendesha siasa za chuki zenye lengo la kuwagombanisha wananchi na serikali badala ya kuwa mstari wa mbele kuhamasisha maendeleo kupitia siasa safi na zenye tija.
“CHADEMA wamechanganyikiwa, kwa sababu siku zote wamekuwa wakitegemea kuendesha chama chao kwa mgongo wa umasikini wa Watanzania, sasa kasi ya kutengeneza ajira kupitia ujenzi wa viwanda, na mchakato wa kuwezesha kuongeza bei ya mazao ili kuwakwamua wakulima kutoka katika umasikini umewachanganya,” alisema Mabula.
Kwa upande wake, Nape aliwaasa wananchi hao kuwapuuza viongozi wa CHADEMA, kwani kazi nzuri inayofanywa na serikali ya CCM katika kuwaletea Watanzania maendeleo imekuwa ikiwakera na ndio sababu wamekuwa wakitafuta njia za kuanzisha vurugu ili kuikwamisha.
Hata hivyo, alisema serikali ya CCM kwa kushirikiana na washirika wake itaendelea kuhakikisha inatekeleza kila ilichoahidi kuwafanyia wananchi, na kwamba hila na ghilba zinazofanywa na viongozi wa CHADEMA kamwe haziwezi kufanikiwa.
Alisema kikubwa kilichowakera CHADEMA ni kuona jitihada za serikali ya CCM na China zinakaribia kuzaa matunda kupitia ujenzi wa viwanda vya pamba, ambavyo pamoja na mambo mengine vitatoa ajira kwa zaidi ya watu 25,000.
Nape, huku akiwa amezungukwa na maelfu ya wananchi katika viwanja vya CCM Sabasaba mkoani Simiyu, alisema mtaji mkubwa wa CHADEMA kisiasa ni tatizo la ajira kwa vijana na kwamba, jitihada za kumaliza tatizo hilo zinazochukuliwa ni pigo kwao, kwani watakosa watu wa kuwaunga mkono kwenye maandamano.
“Tayari tumeshaingia makubaliano na Serikali ya China ya kuwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani ya mazao kama vile pamba, ufuta, alizeti na mazao ya mifugo, ikiwemo ngozi za ng’ombe, hivyo chuki na hasira ya CHADEMA dhidi ya Balozi wa China inasababishwa na mafanikio hayo ya kutatua matatizo ya wananchi,” alisema Nape.
Pia, Nape alionyesha kushangazwa na viongozi wa CHADEMA kulalamika kuhusu kilichofanywa na Balozi Dk. Lu wakati si yeye pekee aliyewahi kuhudhuria shughuli za CCM, ikiwemo Mkutano Mkuu, vikao vya Bunge pamoja na kumtembea Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ofisini kwake, lakini hawakuwahi kupiga kelele kama ilivyo sasa.
‘’Hili ni pigo kwa CHADEMA, kwani watakosa watu wa kuwaunga mkono katika kelele zao na maandamano, mabalozi wengi wamekuwa wakihudhuria sherehe za CCM, ikiwemo kumtembelea Kinana ofisini, zaidi ya nusu ya mabalozi wameshafanya hivyo, mbona hawakupiga kelele na kushitakiwa Umoja wa Mataifa.
“Hili la Balozi Dk. Lu kupanda jukwaani na kueleza kitu gani serikali ya China itakachowafanyia wananchi imekuwa nongwa,’’ alihoji Nape.
Akifafanua, alisema balozi huyo alishawahi kutembelea na kufanya ukaguzi wa ujenzi wa makao makuu ya Chama na Chuo Kikuu cha Chama, Ihemi mkoani Iringa, lakini hakukuwa na malalamiko kutoka CHADEMA.
“Kinachowaumiza CHADEMA ni kuona mtaji wao wa kisiasa wa kuwatumia watu kupiga kelele na kufanya maandamano yasiyo na tija sasa umekwisha,” alisema.
Ends.







Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru