Utouh atuma salamu na mwandishi wetu
MKAGUZI Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, amesema mchakato wa kuanza kukagua hesabu za Manispaa ya Bukoba umekamilika na wiki ijayo kazi itaanza rasmi.
Pia, amewatumia salamu baadhi ya watu waliodai hatakwenda kufanya kazi hiyo kama alivyoagizwa na Rais Jakaya Kikwete, kuwa kwa sasa yuko njiani kwenda Bukoba.
Utouh ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza katika semina ya wahariri, ambapo amesema tayari ameunda timu maalumu itakayofanya kazi hiyo kwa kufuata hadidu za rejea walizopewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo ndio msimamizi wa halmashauri zote nchini.
‘’Tumeshaunda timu maalumu baada ya kupata hadidu za rejea, sasa waambieni watu wa Bukoba waliodhani kuwa hatuendi kuwa tuko barabarani tunawafuata,’’ alisema Utouh.
Ukaguzi huo maalumu unafanyika kutokana na kuibuka kwa madai ya ufisadi unaodaiwa kufanywa na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk. Anatory Amani, hivyo kuzusha mgogoro mkubwa baina yake na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki.
Mgogoro huo ulisababisha kuvuliwa uanachama kwa madiwani wanane, ambapo baadaye ulijadiliwa kwenye Kamati Kuu ya CCM na kisha NEC na kutolewa uamuzi kuwa madiwani hao ni halali, huku baadhi ya viongozi wakipewa onyo kali.
Utouh alieleza kushangazwa na baadhi ya vyombo vya habari (si Uhuru) vilivyodai kuwa, ofisi yake imegoma kufanya kazi, akisema hawezi kufanya hivyo kwa kuwa ni wajibu wake kukagua hesabu za serikali.
‘’Huu ni wajibu wangu, hivyo kamwe siwezi kugomea maagizo ya kiongozi wangu, ninakwenda kuifanya kazi hiyo wiki ijayo na kila kitu kiko sawa,’’ alisema.
Awali, Utouh aliviasa vyombo vya habari kutoa taarifa sahihi kuhusu sera na utekelezaji wa mipango mbalimbali katika ofisi yake, kwani baadhi ya taarifa zimekuwa zikipotoshwa.
Alisema baadhi ama kwa kutambua au kwa makusudi, vimekuwa vikitoa taarifa potofu kuhusu ofisi yake, jambo ambalo ni kuwapotosha wananchi na kuwanyima haki ya msingi.
‘’Wapo ambao huangalia utamu wa kuongeza mauzo, lakini hawatazami athari inayoweza kutokea hapo baadaye. Tumeanza mikakati mbalimbali ya kutoa elimu mbadala kwa wadau wetu ili taarifa zinazotolewa ziwe za uhakika na zenye tija kwa taifa,’’ alisema Utouh.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru