Tuesday 17 September 2013

CCM yawaka


NA SULEIMAN JONGO, MEATU
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amewataka Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki na Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kutoka ofisini  na kwenda maeneo yenye migogoro inayotishia damu kumwagika.
Amesema ni kwa njia hiyo ndipo watakapoweza kumaliza migogoro ya ardhi ya wafugaji na wakulima na ile ya wananchi na maeneo ya hifadhi za taifa.
Kinana aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwasengele kilichoko kwenye jimbo la Kisesa wilayani Meatu Mkoa wa Simiyu akiwa kwenye ziara ya kikazi.
Alisema kuna migogoro mingi maeneo mbalimbali nchini ambayo njia pekee ya kuweza kuitatua ni kwa mawaziri
wanaohusika kwenda kwa wananchi kukaa pamoja na kutafuta suluhu.
Kinana alisema waziri hawezi kutatua mgogoro unaofukuta kati ya wananchi wa Wilaya ya Maswa kuhusu tatizo la maofisa wanyamapori na wafugaji bila kufika eneo husika na kusikiliza kutoka vinywani mwao.
"Kuna migogoro mingi mkoani Morogoro, Wanging'ombe na hapa katika Pori la Akiba la Maswa, lakini ili kuweza kupata ufumbuzi ni lazima kufika kwenye maeneo husika na kusikiliza pande zote, wakiwemo wananchi," alisema.
Katubu Mkuu alisema huu si wakati wa kuendele kutatua migogoro huku mawaziri husika wakiwa ofisini na kuwa sheria zipo kwani hilo
ndilo lililoifikisha migogoro hiyo hapa ilipo.
Aliyasema hayo baada ya kutoa nafasi ya kusikiliza kero za wananchi ambapo mmoja wa waliohudhuria mkutano huo,  Zunzu Ndaturu, alisema kero kubwa inayowakabili wananchi wanaozunguuka pori hilo la hifadhi ni wanyama wakali na maofisa wa hifadhi kuchukua mifugo yao na kuwaomba rushwa mara kwa mara.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kisesa, Luhanga Mpina, alisema licha ya serikali kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ikiwemo kuboresha barabara na ujenzi wa Daraja la Mto Mongo Bhakima uliokuwa kero kwa wakazi wa eneo hilo, bado inaendelea kutekeleza miradi mingine.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru