Wednesday, 18 September 2013

KESI YA MRAMBA NA YONA

NA FURAHA OMARY
MCHAKATO wa kumpata mkaguzi wa madini ya dhahabu ulifanywa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa maagizo ya aliyekuwa Gavana wa Benki hiyo, Dk. Daud Ballali (sasa marehemu), imedaiwa.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa BoT, Kessi-Sia Mbatia (61), alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni waliokuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja.
Mramba na wenzake wanakabiliwa na mashitaka ya kutumia madaraka vibaya na kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 11.7 kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni iliyoshinda zabuni ya ukaguzi wa madini ya dhahabu ya Alex Stewart.
Kessi, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya watu watano walioshughulikia mchakato wa kumpata mkaguzi huyo, alidai hayo mbele ya jopo la mahakimu likiongozwa na Jaji John Utamwa, akiwa shahidi wa Mramba. Mahakimu wengine katika jopo hilo ni Jaji Sam Rumanyika na Saul Kinemela.
Akiongozwa na Wakili Hurbert Nyange, anayemtetea Mramba kutoa ushahidi, Kessi alidai kwa sasa ni mkulima na mshauri mtaalamu, baada ya kustaafu kazi mwaka 2009. Alidai aliajiriwa na BoT tangu mwaka 1975 hadi 2009 kwa  ajira ya kudumu na Desemba 2009 hadi Septemba 2010, alikuwa akifanya kazi kwa mkataba.
Shahidi huyo, alidai kuanzia mwaka 2000 hadi 2005, alikuwa Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa BoT, na kwamba alihusika katika mchakato wa kumpata mkaguzi wa dhahabu kwa maagizo ya Dk. Ballali.
Alidai maagizo hayo alipewa mwishoni mwa mwaka 2002 ya kusimamia kamati aliyoiteua ya watu watano, akiwemo yeye kushughulikia mchakato huo, na kwamba walikuwa wakiwasilisha ripoti kwa gavana.
Kessi alidai wajumbe wa kamati hiyo walikuwa kutoka Wizara ya Nishati na Madini (mmoja), maofisa wa BoT (wawili) na mshauri wa gavana. Alidai kamati hiyo ya awali, baadaye iliongezewa wawakilishi kutoka Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Shahidi huyo alidai kamati ya awali ilifanya kazi ya kuingia katika mtandao kutafuta kampuni za kufanya kazi hiyo, ambapo walipata orodha ya kampuni 21 na baadaye walizichambua na kubaki tano na kuzipeleka taarifa ambapo mbili ziliwasilisha taarifa zao.
ìBaada ya kuchambua taarifa hizo, tulihitimisha kwamba kampuni ya Alex Stewart inastahili kupata kazi hiyo kwa bei ya asilimia 1.9. Tulipeleka mapendekezo yetu kwa gavana ambaye alitutuma kazi, baadaye aliitwa mwakilishi wa kampuni hiyo kufanya makubaliano na hatimaye kupewa mkataba,î alidai.
Sehemu ya ushahidi wa Kessi kwa mtindo wa maswali na majibu akiongozwa na Wakili Nyange ni ifuatavyo:
Nyange; Wakati mnafanya mchakato wa kumtafuta mkandarasi huyo, mlikuwa mnaripoti kwa nani?
Shahidi: Kazi tukimaliza ripoti tunapeleka kwa gavana.
Nyange: Wewe ulikuwa mwajiri wa gavana na gavana alikuwa mwajiri wake nani?
Shahidi: Rais
Nyange: Unamfahamu mshitakiwa aliyesimama (Mramba) na ieleze mahakama unamfahamu vipi?
Shahidi: Ndio, namfahamu kama mwanasiasa na aliwahi kuwa Waziri wa Fedha.
Nyange: Ni kwa kiasi gani mshitakiwa (Mramba) alihusika katika mchakato huo?
Shahidi: Kwa ngazi yangu nisingeweza kujua kwa sababu nilikuwa naripoti kwa gavana na kuishia hapo.
Nyange: Nani alimwalika mwakilishi wa Alex Stewart kuja kufanya makubaliano ya mkataba?
Shahidi: BoT na yalifanywa baina ya kamati na mkandarasi.
Baada ya kuonyeshwa kielelezo ambacho ni mkataba baina ya kampuni hiyo na BoT, shahidi huyo alidai kampuni hiyo ilikuwa iko tayari kuchukua bei ya asilimia 1.9 baada ya kutoa kodi zote.
Pia, alidai kulingana na mkataba mkandarasi huyo ilikuwa afanye kazi kwa miaka miwili, ambapo baadaye aliongezewa miaka miwili mingine kutokana na barua aliyoandikiwa na Gavana Dk. Ballali ya kumteua kuja kutia saini mkataba.
Shahidi huyo alidai mkandarasi huyo alipokuja alikuwa tayari ameshateuliwa, hivyo kamati yao haikuwa na kazi kubwa na hata walipotaka kukaa naye mezani kujadiliana hakuwa tayari kwa madai barua iliyomteua ilimpa haki kama za awali.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo.




Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru