Wednesday 25 September 2013

Babu wa Loliondo aibuka ‘kivingine’


Na Mwandishi Wetu
MCHUNGAJI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwaisapila, amesema Mungu ameendelea kujifunua kwake na kumuonyesha kuwa Tanzania itakuwa kioo cha Afrika na baadaye kioo cha dunia.
Alitoa kauli hiyo juzi asubuhi, mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wakati msafara wa Waziri Mkuu uliposimama nyumbani kwake ili kumsalimia, akiwa njiani kurejea mjini Arusha.
Mchungaji huyo mstaafu maarufu ‘Babu wa Samunge’, alisema kuna mambo mengi ambayo yameandikwa kwenye Biblia, lakini hayakutokea Israel, lakini sasa yatafanyika Samunge.
“Mungu ametupenda mno, yanakuja mambo makubwa na wala hayako mbali. Kama mimi ni mzee na nitayaona, kwa hiyo mtarajie kuwa hayako mbali kutokea,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema katika ufunuo aliopewa na Mungu, ameonyeshwa kwamba watu wengi zaidi watafurika kijijini Samunge kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali kwa misaada iliyotoa wakati wa ‘kugawa kikombe’, ikiwemo mahema, maji na ulinzi.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara maalumu ya kusikiliza matatizo ya ardhi yanayowakabili wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, katika tarafa za Ngorongoro, Loliondo na Sale, alisema anakubaliana na utabiri wa Mchungaji Mwaisapila.
Pinda akithibitisha kuhusu ubashiri wa babu huyo, alisema Tanzania ni nchi iliyojaliwa gesi na mafuta mengi ambavyo vitabadili sura ya nchi.
“Mungu ametupa gesi nyingi mno, katika miaka miwili tutakuwa na umeme kila mahali. Tuna makaa ya mawe ambayo ni nishati kubwa na sasa tuna fursa ya kupata nishati ya umeme kutoka ardhini katika Ziwa Natron,” alisema.
Waziri Mkuu alisema Tanzania imekuwa kimbilio la kila mwekezaji, na kuongeza kwamba sababu kubwa ni amani na utulivu uliopo nchini.
Aliwaeleza wakazi wa Samunge kwamba, mwakani mkandarasi wa barabara atakuwa katika eneo lao kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, ambapo awamu ya kwanza itaanzia Wasso hadi Mto wa Mbu kupitia Samunge.
Akitoa ombi maalumu kwa ajili ya vijana mbele ya Waziri Mkuu, Elias Kalumbwa, alisema wanaiomba serikali iwachimbie bwawa ili waweze kujiajiri kupitia kilimo cha mboga na matunda.
Hata hivyo, Kalumbwa ambaye amesomea masuala ya wanyamapori, alisema eneo hilo liko katika mto wa msimu unaopita kijijini hapo.
“Eneo la kuchimba bwawa liko katika mto wetu, vijana tunaweza kujiajiri, endapo tutapata bwawa ili tufanye kilimo cha umwagiliaji,” alisema huku akishangiliwa.
Naye Bibi Martha Sereri (70) alimweleza Waziri Mkuu kwamba, wanaomba jimbo la Ngorongoro ligawanywe kwa sababu ni kubwa kiasi kwamba inamuwia vigumu mbunge wao kufika maeneo yote.
Pia, bibi huyo aliomba wapatiwe walimu wa masomo ya sayansi na hisabati kwa ajili ya shule 10 za sekondari zilizoko kwenye tarafa yao.
Aidha, alimwomba Waziri Mkuu awaweazeshe kupatiwa mikopo kwa ajili ya ununizi wa matreka ili waweze kuongeza ukubwa wa mashamba yao.
“Tunaomba mikopo ya matrekta na plau, haya mashamba umeyaona njiani yamelimwa na Wakenya. Ukikodisha trekta kila ekari ni sh. 100,000. Je tutafika wapi? Mkitukopesha matrekta mtakuwa mmetusaidia zaidi,” alisema.
Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu alisema hoja zao ni za msingi na kwamba, suala la vijana kupatiwa bwawa inawezekana kupitia Mpango wa Maendeleo ya Kilimo wa Wilaya (DADP).
“Andaeni andiko lenu, inabidi litoke kwa wananchi na siyo serikalini. Mkituletea ni jambo linalowezekana, kwani liko ndani ya mipango ya wilaya.”
Kuhusu ukubwa wa jimbo, Waziri Mkuu aliwaambia wakazi hao kwamba inawezekana kuongeza jimbo isiwe suluhisho la matatizo yao kwa sababu ya jiografia ya eneo lao.
“Kuongeza jimbo inaweza isiwe jibu la kila kitu, kwani matatizo mnayopata yanatokana na jiografia ya eneo lenu, kutoka Ngorongoro, Loliondo hadi huku Sale. Mimi nadhani tuangalie uwezekano wa kuwapa halmashauri ili kusogeza huduma kwa wananchi. Tutaangalia njia zote mbili na kuona ipi italeta majibu ya haraka kwenu,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru