Wednesday 4 September 2013

Chama kilele cha tumbaku chafutwa


Theodos Mgomba na Hamis Shimye.
SERIKALI imekifuta chama kilele cha tumbaku (APEX) hadi pale kitakapoonekana kinahitajika katika kusaidia vyama vya ushirika husika.
Pia, pamoja na kuifuta APEX, imetoa onyo kwa watendaji ndani ya kampuni ya ukaguzi ya Vyama vya Ushirika (COASCO) kuwa, haitasita kuwaondoa watakaoshindwa kuwajibika.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, alipokuwa akihitimisha hoja mbalimbali za wabunge kuhusu muswada wa Sheria wa Vyama vya Ushirika.
Chiza alisema dhana nzima ya uwepo wa APEX ni nzuri, lakini bado matokeo kiutendaji hayakuwa mazuri.
Alisema kama wanachama wenyewe wamepaza sauti ya kutaka APEX iondoke serikali haina budi kusikiliza washirika kwa yale wanayoyataka.
ìTumependekeza kufuta chama kilele ili kutoa nafasi kwa vyama  vikuu na vyama vya msingi kuweza kuwahudumia wakulima kwa ukaribu zaidi, kwani serikali ya CCM ni sikivu,î alisema Chiza.
Akizungumzia juu ya kulegalega kwa ushirika hapa nchini, Naibu Waziri Adam Malima, aliwataka wabunge wasiwe sehemu ya wizi na uozo unaofanyika katika vyama vya ushirika nchini.
Alisema katika sehemu mbalimbali ulikofanyiwa ukaguzi, imeonekana kuna mambo yanapindishwa, huku baadhi ya wabunge wakiwa wanahusika.
ìHumu ndani tunajuana... wengine katika vyama vya ushirika kuna wajomba zetu, kwa hiyo mambo yanapinda pinda bila sababu,î alisema Malima na kuongeza serikali inaangalia uwezekano wa kuongeza adhabu kali kwa viongozi watakaofuja mali za ushirika.
Naibu waziri huyo alisema moja ya masuala hayo ni pamoja na kuangalia sheria ya uhujumu uchumi kutumika kwa viongozi wa aina hiyo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru