Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amesema Tanzania itasimamia vizuri miradi iliyoanzishwa chini ya ufadhili wa serikali ya Marekani na kuhakikisha inakalimika ili iweze kuwanufaisha wananchi waishio maeneo ya miradi husika.
Waziri Mkuu alimshukuru balozi huyo kwa kuiwezesha Tanzania kunufaika na miradi mingi ya kimaendeleo katika kipindi ubalozi huo ulipokuwa chini ya uongozi wake.
ìMiradi uliyoiasisi ni mingi, na kazi uliyoifanya ni kubwa mno. Nimeorodheshewa idadi ya miradi iliyofanyika wakati ukiwa madarakani, kwa kweli ni mingi na orodha ni ndefu mno, tunakushukuru sana,î alisema.
Alisema serikali inapitia upya miradi ya barabara iliyo chini ya MCC ili iweze kunufaisha wakazi wa vijijini kwa kufungua maeneo yao kiuchumi na kuwawezesha kupata masoko kwa urahisi.
Mbali ya barabara, alisema pia serikali imepania kuboresha upatikanaji wa umeme vijijini na wilayani ili kuwezesha uanzishaji wa viwanda vidogo vya usindikaji.
ìLakini jambo hili haliwezi kufanikiwa kama sekta binafsi haitakuwa na mchango mkubwa katika suala hili,î alisema Waziri Mkuu.
Marekani imeisadia Tanzania kwenye miradi ya kuongeza lishe kwenye chakula, kupambana na malaria, afya ya mama na mtoto, ukimwi, kilimo, barabara na nishati.
Kwa upande wake, Balozi Lenhardt alimweleza Waziri Mkuu kwamba amefurahia kipindi chote cha miaka minne ambacho yeye na mke wake waliishi hapa nchini, na kwamba anaamini serikali ya Tanzania itahakikisha miradi yote inayofadhiliwa na nchi hiyo inakamilika.
Alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba miradi yote iliyoanzishwa chini ya uongozi wake inakamilika, na kwamba ana hakika kwamba upatikanaji wake wa fedha hautatetereka kwa sababu yeye anaondoka nchini.
Alisisitiza haja ya sekta binafsi nchini kuhakikisha inashirikiana na serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alimkabidhi Waziri Mkuu zawadi ya sarafu maalum (coin of excellence) ambayo hutolewa kwa watu ambao utendaji kazi wao umetia fora na kumweleza kwamba anatambua mchango wa Waziri Mkuu kwa Taifa hili katika kusukuma suala la kilimo.
Sarafu hiyo ina bendera za Marekani na Tanzania, ina ramani ya Ziwa Victoria na mazao mbalimbali. Waziri Mkuu alimshukuru kwa zawadi hiyo, hasa kwa maana kubwa ambayo sarafu hiyo imebeba.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru