Tuesday 24 September 2013

DC Tarime matatani


NA SULEIMAN JONGO, TARIME
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeingilia kati mgogoro wa muda mrefu kati ya mgodi wa dhahabu wa North Mara, ulioko Nyamongo wilayani Tarime mkoa wa Mara na kuahidi kuupatia ufumbuzi.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele, ametajwa kuwa kinara katika kukuza mgogoro, na kwamba ana maslahi binafsi ndani yake.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, juzi alilazimika kuahirisha shughuli zote alizopangiwa akiwa wilayani humo, ikiwemo baadhi ya mikutano ya hadhara ili kupata muda wa kukutana na pande zote zinazohusika na mgogoro huo.
Kinana alilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka pande mbalimbali, ikiwemo taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM wilayani humo dhidi ya mgodi huo.
Akiwahutubia wananchi wa Nyamongo, Kinana alisema CCM ndicho Chama chenye serikali, hivyo haiwezi kuungana na walalamikaji badala yake imedhamiria kumaliza tatizo hilo.
Alisema tatizo hilo lazima limalizwe mara moja ili wananchi wa Nyamongo na wote wanaouzunguka mgodi huo waishi kwa amani na kunufaika na madini yaliyopo.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ametakiwa kumshauri Rais Jakaya Kikwete, ili aweze kumuhamisha Henjewele ambaye anadaiwa kutafuna fedha za malipo ya ada ya wanafunzi zinazotolewa na mgodi wa Barrick North Mara.
Taarifa ya CCM ya wilaya hiyo iliyosomwa mbele ya Kinana na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kemambo, Rashid Gamaina, ilisema Henjewele amekuwa akichochea mgogoro huo kwa kutoa kauli za kejeli na kuwadhalilisha wananchi wa Nyamongo.
Alisema mkuu huyo wa wilaya alifanya ziara Desemba 31, 2010 katika vijiji vya Nyangoto na Kewanja na kutoa maneno ya kejeli ambayo yaliwadhalilisha watu wa vijiji hivyo.
Kwa mujibu wa Gamaina, mgodi huo uliingia makubaliano na wananchi wanaouzunguka ya kuwalipia ada watoto wao walio kwenye shule na vyuo mbalimbali, jambo ambalo hivi sasa halifanyiki.
“Kitu cha kusikitisha ni kuwa, licha malipo hayo kutositishwa, lakini wanafunzi walengwa hawanufaiki nayo kwa kuwa Henjewele amehamishia malipo hayo ofisini kwake.
“Yeye ndiye anayepanga na kuamua nani, huku akipata fursa ya kufanya mambo ya hovyo, ikiwemo kuwalipia wanafunzi kutoka nchini Kenya badala ya wana Nyamongo kama ilivyokusudiwa,” alisema.
Gamaina alimuomba Kinana kumshauri Rais Kikwete, kumhamisha Henjewele wilayani Tarime kwa kuwa uwepo wake utaendelea kuzorotesha uhusiano wa Chama na wananchi.
Hata hivyo, Henjewele alikanusha madai hayo na kusema fedha zinazotolewa na mgodi kwa ajili ya ada zinawafikia walengwa wote.
Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele aliamuru kusitishwa mara moja kwa mpango huo wa ulipaji ada hadi pale utakapopitiwa na kupangiwa utaratibu mzuri.
Masele alisema baadhi ya viongozi wa ngazi za chini wamekuwa wakiwadanganya wale wa ngazi za juu kwa kuwapa taarifa zisizo sahihi, jambo linalozidisha hasira za wananchi.
Alisema binafsi aliwahi kudanganywa alipotaka kutembelea kijiji cha Nyamongo muda mfupi baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo, huku waliomdanganya wakisema wananchi wa kijiji hicho ni wakorofi na endapo atakwenda amani inaweza kuvunjika.
Kinana aliahidi kumuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani, kufika eneo hilo na kuzungumza na wananchi, ikiwa ni moja ya hatua za kutatua kero zinzowakabili, ikiwemo ya kuwindwa kwa askari wanaolinda mgodi wa Nyamongo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru