Tuesday 3 September 2013

Serikali yavuna bilioni 6.8 mrabaha mazao ya uvuvi


SERIKALI imefanikiwa kupata mrabaha wa sh. bilioni 6.8 kutokana na usafirishaji wa mazao ya uvuvi katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2012/2013.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Benedict Ole Nangoro, alisema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Kombo Khamisi Kombo, (Magogoni-CUF), aliyetaka kujua kwanini serikali imeshindwa kuwekeza katika sekta ya uvuvi.
Nangoro, alisema mapato hayo yanatokana na kuuzwa nje kwa mazao ya uvuvi yenye thamani ya sh. bilioni 254.9, katika kipindi cha mwaka 2012/2013.
Alisema kwa sasa kuna jumla ya viwanda 43 vya watu binafsi vinavyochakata samaki na mazao yake vilivyojengwa nchini.
Aidha, alisema serikali inadhibiti utoroshaji wa mazao ya uvuvi kwa kutumia mifumo ya ufuatiliaji meli wa ‘Vessel Monitoring System, Automatic Information System.’
Naibu huyo, alisema Mamlaka ya kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu, ina uwezo wa kuchunguza taarifa za meli zinazovua katika maji ya Tanzania kinyume cha sheria na kuchukua hatua stahili.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2012/2013, jumla ya meli za uvuvi za kigeni 34 zilipewa leseni za kuvua katika Bahari Kuu na kuiingizia serikali dola za kimarekani milioni 1.305 (sh. tirioni mbili).
“Hata hivyo, tunaendelea kujenga uwezo wa Mamlaka ya kusimamia uvuvi kwa kuipatia vitendea kazi na watumishi zaidi, ili kubaini na kuzikamata meli chache zinazovua na kutorosha mazao ya uvuvi,” alisema.
Nangoro, alisema Wizara ina vituo 21 vya doria vinavyoratibu kwa kushirikisha wadau, kudhibiti uvuvi haramu na utoroshaji wa mazao ya uvuvi kwenye bahari, maziwa makuu, mito, mabwawa, mipakani, viwanja vya ndege na bandarini.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru