Thursday, 18 September 2014

Askari polisi watupiwa bomu Songea


NA MWANDISHI WETU
ASKARI watatu  wa polisi mkoani Ruvuma wamejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa huo mjini Songea, baada ya kushambuliwa  na kitu kinachosadikiwa kuwa bomu la kurushwa kwa mkono.
Tukio hilo lilitokea juzi, jioni katika kata ya Msufini, karibu na daraja la Matarawe, wilayani Songea, mkoani Ruvuma,  ambapo watu watatu wasiofahamika walitupa kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu la kurushwa kwa mkono.
Askari hao walikumbwa na mkasa huo wakati wakiwa kwenye doria katika eneo hilo ni WP. 10399 PC Felista aliyejeruhiwa mguu wa kulia  kwenye unyayo na pajani na G.7351 PC Ramadhani aliyejeruhiwa mguu wa kulia karibu na goti na tumboni .
Mwingine ni  G. 5515 PC John aliyepata majeraha katika mguu wa kulia chini ya goti na jeraha dogo tumboni.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma,  Dk. Daniel Malekela, alithibitisha kuwapokea askari hao na kueleza walitoa  vipande vya bati na misumari katika majeraha yao.
Kutokana na tukio hilo, polisi mkoani Ruvuma wameanza uchunguzi  wa kina ili kuwakamata wahusika.
Akizungumzia tukio hilo,  Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu,  alisema amesikitishwa na kitendo hicho cha wahalifu kujeruhi askari, tena kwa makusudi.
Alisema serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama, itahakikisha wanawasaka na kuwakamata wahusika na hatua zitachukuliwa. Aliowamba wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru