Tuesday, 23 September 2014

Chenge kuwasilisha Katiba Pendekezi Bungeni leo

Na mwandishi wetu, Dodoma

Andrew Chenge
WAKATI wajumbe wa kundi la Katiba ya Wananchi (UKAWA), wakiendelea kususa, Bunge Maalumu la Katiba leo linaingia kwenye hatua muhimu pale Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba, Andrew Chenge, atakapowasilisha Katiba Pendekezi.
Chenge, ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, anatarajiwa kuwasilisha Katiba Pendekezi kwa Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta, baada ya kukamilisha kazi hiyo.
Mara baada ya kuwasilishwa, wajumbe wa Kamati zote 12, watapata fursa ya kuijadili Katiba Pendekezi ili kuwezesha kufanyiwa marekebisho kwenye maeneo, ambayo yataonekana kuwa na upungufu kabla ya  kukabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete.

“Ikirudi kwenye kamati ya uandishi, itaandikwa upya, ikijumuisha hoja mbalimbali, ambazo awali zilikuwa zimeachwa au kufanyiwa marekebisho.
“Kazi hiyo itafanywa kwa siku mbili, kuanzia Septemba 27 hadi 28, mwaka huu,” alisema Sitta alipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana.
Alisema baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, Septemba 29 hadi Oktoba 2, mwaka huu, wajumbe wataanza kupiga kura, wakiwemo wale walioko nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali.
Juzi, Bunge liliridhia na kupitisha Azimio la kufanya marekebisho ya kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, ili kuwaruhusu wajumbe walioko nje ya Bunge, ikiwemo wale walioko nje ya nchi kupiga kura.
JUKWAA LA KATIBA
Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), limesema lina wasiwasi na utaratibu wa kupiga kura kwa wajumbe wa bunge maalumu la katiba watakaokuwa nje ya bunge na nje ya nchi, uliowekwa baada ya kufanyika mabadiliko kadhaa ya kanuni.
Kanuni zilizofanyiwa marekebisho na bunge hilo linalotarajiwa kuhitimisha kazi yake, ni tatu ambazo lengo kuu lilikuwa ni kurahisisha zoezi la upigaji kura ndani ya bunge hilo, litakaloanza Septemba 29, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa JUKATA, Deus Kibamba, hatua hiyo inatakiwa kuangaliwa kwa makini ili kuondoa dhana ya baadhi ya watu kuwa ni moja ya njia za kuchakachua mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya.
Ilisema baadhi ya mambo ya kuyaangalia kwa undani ni pamoja na gharama za kuendesha mfumo huo, unaotegemewa kufuatwa kutokana na marekebisho ya kanuni namba 30, 36 na 38 za bunge hilo maalumu la katiba.
Aidha, taarifa hiyo ilishauri kutafutwe njia mbadala ya kutafuta theluthi mbili ya wajumbe wa bunge hilo maalumu la katiba, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wajumbe wanaoruhusiwa kupiga kura watakuwa wale tu walioko ndani ya bunge hilo katika tarehe husika ya zoezi hilo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru