Thursday, 11 September 2014

Waumini wa Sunni Jamaat wamvaa Turki


Na Mwandishi Wetu
WAUMINI wa Jumuia ya Sunni Muslim Jamaat, Dar es Salaam, wamemtaka mbunge wa Mpendae-CCM, Salim Turki, kufuata utaratibu na kuacha kuwanyanyasa waumini wenzake.
Imedaiwa kuwa Turki amekuwa akifanya vitendo vinavyokwenda kinyume na huwatisha waumini wenzake kuwa hakuna wa kumfanya lolote kwa kuwa ni mbunge.
Wakiunguza na waandishi wa habari jana, waumini hao walidai kuwa Turki amekiuka maagizo ya Mahakama Kuu iliyozuia uchaguzi wa jumuia hiyo hadi pande mbili zinazovutana zitakapokutana na Ofisi ya Mrajisi ili kuhakiki wajumbe.
Hata hivyo, Turki alilazimisha kufanyika kwa uchaguzi huo huku akiwatumia polisi kuwadhibiti waumini, jambo ambalo limezusha malalamiko.
Uchaguzi huo ulifanyika Agosti 8, mwaka huu, katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, ambapo ulifanyika chini ya ulinzi mkali wa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia(FFU).
Mmoja wa waumini hao, Ahmadia Mohammed, alisema mbunge huyo amekuwa tatizo kwenye jumuia hiyo huku akitumia wadhifa wake huo kisiasa kama ngao.
Alipotafutwa kuzungumzia madai hayo, Turki hakuwa tayari kupokea simu yake ya kiganjani na alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu, alijibu kuwa yuko kikaoni.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru