Wednesday, 10 September 2014

Vijana Kibaha watakiwa kugombea uongozi

NA MWANDISHI WETU
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kibaha Mjini, kimewataka vijana kuthubutu kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika ucaguzi ujao wa Chama na serikali.
Mwenyekiti wa UVCCM Kibaha Mjini, Idd Kanyalu, aliyasema hayo juzi,  katika eneo la Mzizizma  Zegereni, kata ya Visiga, alipokuwa akizungumza na wananchi, wakati wa ziara ya kamati ya maboresho inayolenga kukagua uhai wa jumuia hiyo.
Kanyalu aliwaasa vijana hao kujipanga kwenye mchakato wa uchaguzi kuanzia serikali  za mitaa, ili kuhakikisha wagombea wote wanaosimamishwa na chama hicho wanashinda kwa kishindo.
Aidha Kanyalu aliwataka vijana, hususan wajasiriamali, kuacha tabia ya ubinafsi,  badala yake wajiunge na vikundi ili waweze kupata fursa za kimaendeleo na kupatiwa mikopo kwa urahisi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maboresho, Hamza Duluge, aliwataka vijana na wananchi kutokubali kurubuniwa  na wanasiasa kutoka nje ya CCM .
Alisema wanasiasa hao hawaonekani katika kipindi chote, lakini uchaguzi unapokaribia, wanajitokeza na kuanza kuwarubuni wananchi.
Kwa upande wake Katibu wa kamati hiyo Nicolaus Maliga, alisema ni wakati mwafaka kwa vijana kujitambua na kutokubali kutoa mwanya kwa watu wachache nje ya chama hicho, wenye lengo la kutaka madaraka wakitumia fursa ya kuwagonganisha ili watimize malengo yao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru